Rais aanguka tena kwa kizunguzungu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Lusaka

Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mheshimiwa Edgar Lungu ameanguka akiwa katika maadhimisho ya 45 ya Siku ya Ulinzi Kitaifa nchini humo.

Hali hiyo ilitokea Juni 13, 2021 ambapo alilazimika kusitisha kila kitu na kurejea ofisini kwake katika Ikulu iliyopo mjini Lusaka.

Mwakilishi wa Diramakini Blog Ukanda wa Kusini mwa Afrika, amebainisha kuwa, Mheshimiwa Rais Lungu alipata kizunguzungu cha ghafla kama kilichomtokea miaka sita iliyopita na kuondolewa eneo la tukio mara moja na maafisa usalama.

Akizungumzia kuhusiana na hali hiyo, Katibu wa Baraza la Mawaziri, Dkt.Simon Miti amesema kuwa,baada ya hali hiyo Mheshimiwa Rais alirejea Ikulu na anaendelea vizuri kiafya.

“Rais wa Jamhuri ya Zambia,Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, mchana wa leo amejikuta katika hali ya kizunguzungu akiwa katika maadhimisho ya 45 ya Siku ya Ulinzi Kitaifa. Hali ya Mheshimiwa Rais ilirejea vizuri haraka na kuelekea katika gari lake kurejea katika makazi yake kule Ikulu,"ameeleza Dkt.Miti.

Amesema, Rais anauhakikishia umma kuwa, afya yake inaendelea vizuri na anaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida kama Mkuu wa nchi.

“Mheshimiwa Rais anapenda kuuhakikishia umma pamoja na jumuiya ya Kimataifa kwamba ni mzima wa afya, hivyo anaendelea kutekeleza majukumu yake kama Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,"ameongeza Dkt.Miti.
Miongoni mwa raia wa Zambia kutoka mjini Lusaka aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Chawezi ameieleza DIRAMAKINI Blog kuwa, kuna haja ya Rais wao kupata muda wa kupumzika zaidi na kupata matibabu ya kutosha kwa kuwa, tukio kama hilo limewahi kuzua hofu mwaka 2015 katika uwanja wa Heroes National Stadium mjini Lusaka.

Tukio hilo lilitokea Jumapili ya Machi 8, 2015 ambapo Mheshimiwa Rais Edgar Lungu alianguka wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika majira ya asubuhi, hivyo Waziri wake wa masuala ya Jinsia,Prof. Nkandu Luo akaendelea kumuwakilisha.

Kiongozi huyo ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi alilazimika kuondoka ghafla uwanjani hapo ambapo baadaye, Msaidizi wake, Amos Chanda alisema kuwa, siku hiyo alikuwa mchovu kutokana na ugonjwa wa malaria ambao ulikuwa unamsumbua.

Bado kuna hali ya wasiwasi kuhusiana na afya ya Rais Edgar Lungu ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka sita sasa, kufuatia kifo cha mtangulizi wake Michael Charles Chilufya Sata.

Rais Sata alifariki dunia Oktoba 28, 2014 wakati akiendelea na matibabu ya maradhi ambayo yalikuwa yanamkabili huko jijini London, Uingereza.

Baada ya kifo cha Sata, Mheshimiwa Lungu alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo kutumikia muda alioubakisha mtangulizi wake mpaka kufikia sasa ambapo harakati za uchaguzi Mkuu zinaendelea nchini humo.

Post a Comment

0 Comments