RAIS SAMIA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA DARAJA LA JPM MKOANI MWANZA

Na Deniza Cyprian

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM linalojengwa katika eneo la Kigongo hadi Busisi jijini Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipokuwa akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Km 3.2), mkoani Mwanza.

Akizungumza na wananchi upande wa Sengerema mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja hilo, Rais Samia alisema kuwa nia ya Serikali ni kulifanya jiji la Mwanza kuwa Kitovu cha Biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.

“Daraja la JPM litarahisisha huduma za usafiri na pia kupunguza muda wa kuvuka katika Ziwa hilo tofauti na ilivyo sasa ambapo wasafiri wanatumia muda mrefu kusubiri kivuko na ili kupata huduma ya kuvuka,”amesema Rais Samia.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alimuahidi Rais Samia kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia ujenzi wa Daraja la JP Magufuli kwa karibu ili kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba ili wananchi waweze kunufaika na mradi huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mheshimiwa Rais naomba nitumie fursa hii kukukaribisha katika eneo la mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli. Wizara inashirikiana vizuri na wenyeji wa eneo hili katika kuendeleza mradi huu ambapo hadi sasa ajira kwa ajili ya usaidizi wa ujenzi wa daraja hili zimetolewa kwa wakazi wa hapa Sengerema, Misungwi pamoja na maeneo mengine ya jiji la Mwanza, hivyo wakazi wa eneo hili tayari wameanza kuonja matunda ya mradi huu,”amesema Dkt. Chamuriho.

Awali akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, alimueleza Rais Samia kuwa Daraja la JPM lenye urefu wa Kilometa 3.2 na upana meta 28.45 ambalo pia linahusisha ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa Kilometa 1.66 linagharimu shilingi Bilioni 716 na kwamba hadi sasa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 27.

“Mheshiwa Rais kama utakavyojionea daraja la muda tayari limekamilika kwa asilimia 100 na sasa magari yanaweza kuvuka kwenda Busisi na kurudi, daraja hili la muda limejengwa kwa ajili ya kurahisisha shughuli za ujenzi wa daraja kubwa,”ameeleza Mhandisi Mfugale.

Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo kukamilika kwake kutarahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani mikoa ya Mwanza, Geita pamoja na nchi jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news