Rais Samia:Tutaendelea kukuza uhusiano, ushirikiano na Botswana

Na MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Botswana, Dkt.Mokgweetsi Masisi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hiyo hususan katika kukuza biashara na uwekezaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi kabla ya kuanza mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 10, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais Dkt.Masisi ambaye alianza ziara ya kikazi ya siku mbili hapa nchini kwa mualiko wa Rais Samia.

Rais Samia amesema, Botswana na Tanzania zina uhusiano wa kidugu na kihistoria ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Botswana Hayati Seretse Khama hivyo hakuna sababu kwa nchi hizo kuwa na kiwango kidogo cha biashara ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanahabari mara baada ya mazungumzo yao Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi Ikulu Jijini Dar es Salaam

Amefafanua kuwa, mwaka 2018 biashara kati ya Tanzania na Botswana ilikuwa kutoka shilingi milioni 731 hadi shilingi Bilioni 3.5 na kwamba Botswana imewekeza hapa nchini kiasi cha dola za Marekani Milioni 231 zilizoajiri Watanzania 2,128.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi wakati wakielekea kwenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya mazungumzo rasmi Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.  

Rais Samia amesema, katika kukuza uhusiano huo Tanzania ipo tayari kushirikiana na Botswana katika kuboresha ufugaji, kunufaika na uwekezaji wa madini hususan almasi, kukuza utalii na kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vya Botswana.

Amemhakikishia Rais Masisi kuwa Tanzania italinda uwekezaji wowote kutoka Botswana kwa manufaa ya pande zote mbili na amewasihi wawekezaji kutoka Botswana na kwingineko duniani kuja nchini Tanzania kuwekeza kwa kuwa mazingira ya uwekezaji ni mazuri.

Rais Samia amewataka mawaziri na wataalam wa Tanzania na Botswana kufufua kamati ya kudumu ya pamoja (JPC) ambayo haijakutana tangu mwaka 2009 kukutana haraka iwezekanavyo ili kupitia maeneo yote ya ushirikiano na kuongeza maeneo mapya kwa manufaa ya pande zote mbili. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na Ujumbe wa Botswana uliokuwa ukiongozwa na Rais wao Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Kwa upande wake Rais Masisi amemshukuru Rais Samia kwa kumualika kuja hapa nchini, alimpongeza kwa kupokea kijiti cha urais na alimuhakikishia kuwa yupo tayari kumpa ushirikiano wowote atakaohitaji na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Botswana.

Rais Masisi amesema, kutokana na uhusiano mzuri, udugu na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Botswana nchi hizo hazina budi kudumisha amani na utulivu ili kutoa nafasi ya kukua kwa uchumi na ustawi wa wananchi wake. Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi akizungumza na Wanahabari Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021. (PICHA NA IKULU).

Ameongeza kuwa, Botswana iko tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya madini hususan almasi, ufugaji na utafutaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali.

Rais Dkt.Masisi ameungana na Rais Samia kutaka JPC ikutane ndani ya miezi mitati na alimualika Rais Samia kufanya ziara rasmi nchini Botswana.

Hata hivyo,leo Mhe. Rais Masisi atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Samia kwa heshima yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news