Simba SC yawapiga kanzu Yanga SC, Azam FC Ligi Kuu Tanzania Bara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

This is Simba! Ndiyo unavyoweza kusema, baada ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kuuendeleza ubabe katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ni baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Mbeya City katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashuri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Katika mtanange huo wa Juni 22,2021 mabao ya Simba SC yamefungwa na Rally Bwalya dakika ya 31, Luis Miquissone dakika ya 35.

Mengine yamefungwa na Nahodha John Bocco dakika ya 47 na Clatous Chama dakika ya 86, wakati la Mbeya City limefungwa na Pastory Athanas dakika ya 51.

Kwa matokeo haya, Simba SC inafikisha alama 73 baada ya ushindi huo na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa alama sita zaidi ya mahasimu wao, Yanga SC ambao pia wamecheza mechi mbili zaidi.

Nao Mbeya City baada ya kupoteza mchezo huu katika mechi ya 32, wanabaki na alama zao 36 katika nafasi ya 13.

TANZANIA PRISONS VS COASTAL UNION

Wakati huo huo, Tanzania Prisons imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Coastal Union.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Mandela lililopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Tanzania Prisons mabao yake yamefungwa na Samson Mbangula dakika ya 19 na Jeremiah Juma dakika ya 36.

Kwa upande wa Coastal Union mabao yao yamefungwa na Abdul Suleiman kwa penalti dakika ya 23 na Mudathir Said dakika ya 85.

Tanzania Prisons kutokana na matokeo hayo inafikisha alama 42 baada ya kucheza mechi 32 na kusogea nafasi ya saba kutoka ya tisa.

Wao Coastal Union wanafikisha alama 34 za mechi 31 sasa.

Aidha, wanabaki nafasi ya 16 katika ligi ya timu 18 ambayo mwishoni mwa msimu tatu zitashuka.

AZAM FC VS NAMUNGO

Awali Azam FC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika dimba la Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Sare hiyo inayoiongezea kila timu alama moja na inaifanya Azam FC ifikishe alama 64.

Ni baada ya kucheza mechi 32 sasa, ingawa inabaki nafasi ya tatu ikizidiwa alama tatu na Yanga SC.

Kwa upande wa Namungo FC inafikisha alama 43 za mechi 32 pia na inabaki nafasi ya tano ikizidiwa alama sita na Biashara United ya mkoani Mara.

KMC awali imelazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar katika dimba la Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Mtibwa Sugar ilitangulia kwa bao la Kelvin Sabato dakika ya 55, kabla ya wenyeji KMC FC kusawazisha kupitia kwa Cliff Buyoya dakika ya 82 katika mtanange huo safi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news