Unayopaswa kuyafahamu kwa kina kuhusu Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)

NA DIRAMAKINI

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).

Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.

TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.

Kwa mujibu wa tume hiyo, viasili vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Hivyo, sababu kuu za kupima mionzi katika mnyororo wa chakula ni kuhakikisha chakula kinacholiwa na Watanzania hakina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.

Pia ni muhimu kuhakikisha kuwa soko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinalindwa ili kuzingatia ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na miongozo na taratibu mbalimbali za Serikali.

Miongoni mwa sababu zinazosababisha upimaji wa mionzi ni kutokana na ukweli kuwa, usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking) unaweza kusababisha uchafuzi kwenye vyakula na mazingira.

Sababu nyingine kwa mujibu wa TAEC ni kuwepo kwa mionzi asili kwenye udongo na mazingira yetu kama vile madini ya urani katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia kila mmoja wetu anatambua kuwa, ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi, hivyo kupitia tume hiyo imechukua hatua za kulinda mnyororo mzima wa chakula ili wananchi wake wawe salama

Sambamba na kulinda soko la bidhaa zetu zinazouzwa nje ya Tanzania hasa wakati huu wa vita ya kiuchumi. Upimaji unatoa uwezekano wa kufuatilia kama kuna shida yoyote ikiewemo kutekeleza takwa la kisheria, kupima mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama ilivyoahinishwa kwenye Sheria Na. 7 ya Mwaka 2003.

Sheria hii inaendana na matakwa ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).

Wataalam TAEC kazini muda wote

Kwa kuzingatia umuhimu wa tume hii katika kuangazia udhibiti matumizi salama ya mionzi, imepewa kibali na mamlaka ya kuhakikisha mitambo inayokuja hapa nchini kwa ajili ya kufanya kazi za kutoa mionzi hususani mashine zinazotumika Sekta ya Afya kupimia saratani,wataalamu wa tume wanahakikisha wanachunguza mitambo hiyo ili kubaini kama ni salama ili isiweze kuleta madhara kwa Watanzania.

Pia wanahusika kusimamia migodi,viwanda na maeneo mbalimbali ambayo yana vyanzo vya migodi ili kuhakikisha havileti madhara kwa wananchi.

Ufanisi wa kazi bora za TAEC unatokana na vitendea kazi vya kisasa ikiwemo mahabara za kisasa ambazo zinapatikana katika tume.
Wanafunzi wa Kidato cha Nne kutoka katika Shule ya Sekondari ya Elerai ya jijini Arusha wakipata maelezo kutoka kwa Mtafiti wakati wa ziara yao katika Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ili kupata elimu kwa vitendo katika mahabara ya Uhakiki wa Vifaa vya Mionzi. Ziara hiyo imefanyika Juni 7,2021.

Tume kwa kutambua umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo na kuwapa hamasa wanafunzi wa Kitanzania kusomea masomo ya sayansi imeendelea kutoa fursa kwa wanafunzi kufika kwao kujifunza kwa vitendo yale wanayofundisha ikiwemo Shule ya Sekondari Erelai jijini Arusha.

Wanafunzi mbalimbali wamekuwa wakifika kujifunza jinsi ambavyo wanaweza kupata manufaa ya uwepo wa tume hiyo na kujifunza kwa vitendo wanayosoma darasani.

Miongoni mwa watafiti wa nyukilia kutoka TAEC anasema kuwa, jukumu walilopewa ni takwa la kisheria ambalo linawataka kuhakikisha wanatoa uwezo kwa kada mbalimbali kutambua kwamba tume hiyo ya nguvu za atomiki Tanzania haihusiki kabisa kutengeneza mabomu bali inahusika kulinda wananchi wa Tanzania juu ya matumizi salama ya mionzi na kuendeleza teknolojia ya nyukilia na ni zoezi endelevu.

TAEC inajivunia kwa uwezo wanaojengewa na Serikali ambao umeifanya kuwa ni tume pekee kwa upande wa Afrika ya Mashariki na Kati yenye mitambo ya kisasa ambayo husaidia sana wananchi kuwa salama na ukizingatia kwamba shughuli nyingi za Serikali utegemea mionzi hiyo ya asili na ya kutengeneza.

"Kuna maabara nane za kisasa ambazo zipo katika tume hii zinazotumika kupima kiwango cha mionzi kinachoweza kuingia kwenye mwili wa binadamu, kwa mfano mtu anayefanya kazi sekta ya afya na migodi, tume ina vifaa maalumu ambavyo tunawapa kuvaa kifuani, wanapokuwa kwenye majukumu yao na baada ya miezi mitatu wanavituma kwenye tume kuvipima kuona ni kiwango gani cha mionzi kinaingia ndani ya miili yao, lengo ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanaofanya kazi katika sekta hizo hawadhuriki,"anabainisha Mtafiti kutoka TAEC.

Mapokezi na maelezo mazuri kutoka kwa wataalam wa TAEC, yamewafanya wanafunzi wanaofika kujifunza kutamani kuendelea kukaa katika maeneo ya tume muda wote,huku wakitumia muda mwingi kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TAEC kwa namna ambavyo ilivyowekeza vifaa vya kisasa na wataalam wabobezi ambao wapo tayari kwa ufafanuzi mzuri na kutoa majibu ambayo yanawapa mwanga wa kutamani kusoma masomo ya sayansi.

Wanafunzi wanasema, kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa na kwamba baadhi ya mashine walikuwa wanazisoma darasani tu, lakini jambo la kufurahisha wameziona kwa macho yao na kuonyeshwa kwa vitendo na jinsi zinavyoweza kufanya kazi na kuleta tija kwa Taifa .

Aidha, wanasema wanaipongeza TAEC kwa kuwa na mitambo mikubwa ambayo inaweza kupima kiwango cha mionzi katika vyakula kutoka nje ya nchi huku wakishirikiana vyema na taasisi mbalimbali za Serikali hususani Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) kujua kama muhusika ana kibali na kuhakikisha kwamba watanzania na wananchi hawapati madhara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news