NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mchungaji Peter Msigwa ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini mkoani Iringa na aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini mkoani Mbeya, Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr.Sugu wamefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Kamishna wa Magereza Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Uamuzi huo wameufikia wakipinga kile ambacho wanadai ni kukiukwa kwa haki zao za msingi na kikatiba wakati wanatumikia adhabu walizopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya jijini Mbeya.
Tumaini amesema kuwa, Juni 15,2021 kesi hiyo inatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, ikiwa chini ya jopo la majaji watatu na mawakili wa upande wa utetezi zaidi ya 15.Amesema,katika kesi hiyo madai yapo mengi, lakini yamewekwa katika sehemu tatu ambapo ni kulalamikia sheria za Magereza ambazo amedai zimepitwa na wakati.
Pia utamadumi wa namna ambavyo Jeshi la Magereza limekuwa likifanya kazi zao pamoja na sheria nyingine za nchi.
Amesema, lengo la kesi hiyo wanaamini kila mtu ni mfungwa mtarajiwa, hivyo wana jukumu la kuleta mabadiliko na mifumo ya sheria nchini.
Mchungaji Msigwa amesema wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Magereza Tanzania wakipinga kukiukwa kwa haki zao za msingi na za kikatiba wakati wakitumikia adhabu walizopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.
Amedai, yeye mwenyewe (Mheshimiwa Peter Msigwa) na viongozi wenzake walikuwa tunakabiliwa na kesi ya Jinai ya Mwaka 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukamilika kwa kesi hiyo Machi 10,2020 walipatikana na hatia na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 40,000,000 au kutumikia kifungo cha miezi mitano jela.
