BITEKO:BUCKREEF IKUTANE NA WANANCHI

Na Tito Mselem, Dodoma

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Backreef imesisitizwa kukutana na wananchi wanaozunguka eneo la Leseni ya kampuni hiyo ili kupanga na kujua mahitaji ya wananchi kabla hawajashiriki katika utoaji Huduma kwa Jamii (CSR).
Kauli hiyo, ameitoa Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Juni 23, 2021 kwenye kikao chake na uongozi wa Kampuni ya Backreef kilichofanyika katika ukumbi wa Prof. Abdukarim Mruma jijini Dodoma.

Kampuni ya Buckreef inayojishughulisha na Uchimbaji wa Madini ya dhahabu katika mkoa wa Geita inashirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo Kampuni ya Buckreef inamiliki hisa kwa asilimia 55 na STAMICO asilimia 45.

Waziri Biteko amesema Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 inaeleza wazi kuwa, Mwekezaji katika shughuli za madini lazima ashirikiane na wananchi kuamua mradi gani unahitajika kwa jamii husika ili utekelezwe kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, Waziri Biteko amewapongeza viongozi wa Kampuni ya Buckreef kwa hatua nzuri iliyofikiwa ambapo mpaka sasa wameishafanya tathmini kwa baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka leseni ya mgodi huo kwa lengo la kutoa fidia kwa wananchi.
Sambamba na hapo Waziri Biteko amewataka viongozi hao wakamilishe mahitaji yanayotakiwa kwa haraka ili uzalishaji uanze kwa wakati.

“Niwaombe viongozi wa Buckreef muhakikishe mnalipa watu kwa wakati, mwenye mazao yake alipwe, mwenye nyumba yake alipwe na mwenye eneo lake alipwe ili shughuli za uzalishaji zianze,” amesema Waziri Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula amesema, Serikali za Mitaa lazima ithibitishe huduma ya jamii inayotolewa kwa jamii husika.

Vile vile, Prof. Kikula amewataka viongozi wa Buckreef kupunguza muda wa kukamilisha hatua zinazotakiwa kukamilishwa ili uzalishaji uanze ambapo itasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa watanzania na kuipatia kodi Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news