TEF YAIPONGEZA SERIKALI KWA MUUNDO WA BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI

Na Beatrice Sanga, MAELEZO, Morogoro

Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF limeipongeza Serikali kwa kuweka Bodi ya Ithibati kwenye sheria ya huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo itasaidia kuleta maadili ya Mwandishi wa Habari moja kwa moja badala ya ilivyo sasa ambapo sheria hukiwajibisha chombo cha habari kwa makosa ya Mwandishi.

TEF imesema Bodi hiyo ya Ithibati inayotarajiwa kuanza mapema mwakani, itasaidia pia kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyombo vya habari kutokana na kuwa na uwezo wa kutoa adhabu kwa Waandishi na Wahariri wao watakaokiuka sheria na kanuni za uandishi wa habari.
Picha mbalimbali zikionesha Wadau wa kupigania haki za Waandishi wa Habari Wanawake wakiwa katika Mkutano wa Siku nne Mkoani Morogoro wakijadili na kupanga mradi wa kuimarisha nafasi ya vyombo vya Habari katika kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto pamoja na wadau wa maendeleo kutoka katika mashirika ya kimataifa, asasi zisizo za kiserikali na Taasisi za Umma. (Picha na MAELEZO).

Akizungumza katika mkutano wa siku nne wa kupanga mradi wa kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari katika kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, na Wadau wa kupigania haki za Waandishi wa Habari Wanawake unaoendelea Mkoani Morogoro, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF Bw. Neville Meena amesema kumekuwa na changamoto nyingi kwenye vyombo vya habari na kwamba ujio wa Bodi hiyo utajibu na kutatua changamoto hizo.

“Bodi ya Ithibati itaondoa unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyombo vya habari kwa sababu itahusika na Mwandishi moja kwa moja kwa kurekebisha makosa ambayo hayapaswi kufanywa, pia italeta weledi katika kusimamia maadili, kwani changamoto iliyopo sasa ni kwamba, endapo Mwandishi anakiuka maadili, kinahukumiwa chombo, hili kwetu sisi tunaliona ni tatizo,” amesema Meena.

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa na weledi na sasa Waandishi pia watatakiwa kuwa katika hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboreshewa maslahi yao pamoja na Mazingira bora ya kazi zao.

Kuhusu nafasi ya Wanawake kwenye vyombo vya habari, Meena amesema Wanawake wengi waliopewa nafasi za uongozi katika vyombo hivyo wanafanya kazi nzuri na wanapaswa kupongezwa.

“Tuna mifano mingi ya Wanawake waliopata nafasi za uongozi katika vyombo vya habari, wanafanya kazi nzuri sana,tuwatie moyo na Wanawake wengine zaidi kwenye suala hili,” amesema Meena.

Nae Mkurugenzi Msaidizi Usajili upande wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Patrick Kipangula amesema bodi hiyo imetumwa kupitia Sheria namba 12 ya mwaka 2016 lengo likiwa ni kuwapa fursa wanahabari kuamua mambo yao.

Chimbuko la mkutano huo ni maazimio ya Mkutano wa Siku ya uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambao Kitaifa ulifanyika Jijini Arusha Mei 3 mwaka huu wa 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news