Awamu ya Sita na ujio wa Bima ya Afya kwa Wote, Waziri Gwajima abainisha mengi

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

SERIKALI ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote na kuwahakikishia wananchi wote huduma za afya wakiwemo wasio na uwezo wa kugharamia matibabu.
Kadhalika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga sh.Bilioni 149 kwa ajili ya kugharamia bima kwa kwa wasio na uwezo wa kugharamia matibabu.
Hayo yamebainishwa leo jijini hapa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto,Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF.

Amesema, sheria hii inalenga kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya na kwamba kutokuwa na fedha au uwezo wa kuchangia huduma za matibabu isiwe kikwazo cha mwanananchi kupata huduma za afya.

“Utekelezaji wa jambo hili unaenda vizuri na kama mlivyomsikia Waziri Mkuu alipokuwa akisoma hotuba ya kuwasilisha hoja ya kuhitimisha bunge alisema serikali imejipanga kuwasilisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote kwenye bunge la Septemba, mwaka huu.

"Kwa dhamira hii njema ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia tayari ajenda hii imepiga mbio kubwa na kufikia kwenye hatua ambayo tunamalizia na kuingia kwenye utekelezaji,”ameeleza.

Waziri Dkt. Gwajima amesema katika kusherehekea miaka 20 ya kuanzishwa kwa NHIF kunatoa nuru kuanza kujipanga zaidi kuwafikia wanachama na kuwasikiliza mahitaji yao na itasaidia kuboresha zaidi na kuufanya mfuko kuwa bora zaidi.

“Wekeni mipango madhubuti wa kushughulikia changamoto ambazo mmekabiliana nazo katika kipindi hiki ili ziwe chachu ya kufikia mafanikio na lengo la serikali la kila mtanzania kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya.

“Tumieni kipindi hiki cha siku 90 za maadhimisho kutoa elimu zaidi na kuhamasisha wananchi hususani wa vijijini ili waweze kuona umuhimu wa bima ya afya na kujiunga,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga amesema, kwa kipindi cha miaka 20 ya utoaji huduma NHIF imeongeza wigo wa kutoa huduma kwa kuendelea kusajili vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 3,198 wakati inaanzishwa hadi vituo 8,970 Juni 2020.

Konga amesema katika kupanua wigo wa wanachama mfuko umejumuisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wabunge, Wajumbe wa baraza la wawakilishi, Wajasiriamali, Wafanyakazi wa Kampuni Binafsi na Wanafunzi wa vyuo.

“Idadi ya wanachamna na wachangiaji imeongezeka kutoka wanufaika 691,774 mwaka 2001 hadi kufikia wanufaika milioni 4.3 mwezi Machi 2021 sawa na asilimia nane ya watanzania wote,”ameeleza.

Naye Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya NHIF, Juma Muhimbi amesema katika kuhakikisha mfuko unaendelea mbele zaidi wamejipanga kuhakikisha wanawasikiliza wanachama kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

“Nampongeza Rais Samia kwa kuniteua mimi kushika nafasi hii ninaamini nitafanya yale yote ambayo yananipasa kufanya ikiwa ni pamoja na kushirikiana na timu ya wajumbe wangu ili gurudumu hili lifike mbali zaidi,”ameeleza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news