Dkt.Sengati aitaka TASAF kuhakikisha walengwa wanakidhi vigezo kisheria

Na Anthony Ishengoma, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Philemon Sengati amesisitiza agizo la Serikali kwa TASAF la kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu mpango wake wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF ya kunusuru kaya masikini kuhusu namna ambavyo wanufaika wanapatikana ili kuondoa malalamiko katika jamii ambayo yalijitokeza kwa kiwango fulani katika awamu za awali.

Dkt.Sengati pia ameitaka TASAF kuhakikisha wasimamizi wa zoezi la utambuzi wa wanufaika wa TASAF wa mpango wa pili wa awamu hii ya tatu wanakuwa ni wale tu waliokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

Ameyasema hayo wakati alipozindua kikao kazi cha wadau waliofika katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga kupata elimu ya kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya utoaji ruzuku na TASAF kwa kaya masikini mkoani Shinyanga.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF Nchini Bw. Japhet Boaz akiwapitisha wadau wa TASAF Mkoa wa Shinyanga waliofika katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga kushiriki uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya utoaji ruzuku na TASAF kwa kaya masikini.

Dkt.Sengati ameongeza kuwa, utekelezaji wa mpango wa TASAF ni moja ya nyenzo ya kupambana na umasikini akiongeza kuwa zaidi ya kaya milioni moja zimewezeshwa na TASAF kupambana na umasikini kwani wapo ambao wameanzisha miradi ya ujasiriamali inayowasaidia kuendesha maisha kwa unafuu zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa hapo mwanzo.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAF nchini, Japhet Boaz amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa TASAF katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu inalenga kuzifikia kaya masikini ambazo hazikuguswa katika awamu zilizopita na kuitaka jamii kutambua kuwa miradi ya TASAF siyo ya kudumu kwani wanufaika watahitaji kuhitimu.

Boaz aliongeza kuwa, Mkoa wa Shinyanga una jumla ya vijiji na mitaa 247 ambayo haijafikiwa na TASAF, hivyo katika kipindi hiki miradi ya TASAF inalenga kuwafikia wananchi wanaoishi katika vijiji na mitaa hiyo kwa lengo la kutoa ruzuku kwa kaya ya masikini. Wadau wa TASAF Mkoa wa Shinyanga waliofika katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga kushiriki uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya utoaji ruzuku na TASAF kwa kaya masikini.

Alizitaja familia zitakazonufaika ni pamoja na zile zenye watu walemavu, familia zinazoendeshwa na watoto yatima pamoja na kuwawezesha watoto wa kaya masikini kwenda kliniki ikiwemo kuwawezesha kwenda shule kuanzia shule ya awali mpaka sekondari.

Wakati huo Msimamizi wa TASAF Mkoa wa Shinyanga, Doto Maligisa alisema, changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa Miradi ya TASAF Shinyanga ni kuhama kwa baadhi ya kaya za wanufaika na wamekuwa wakifanya hivyo bila kutoa taarifa za kule walikohamia.

Doto alitoa wito kwa wanafamilia hao kutoa taarifa kwa serikali za vijiji walikohamia na kujitambulisha kwa kutoa kitambulisho cha TASAF ili uko waliko waweze kuendelea na kupata huduma za TASAF ili kuepukana na hadha ya kuendelea kubaki katika umasikini. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akiwa na katika picha ya pamoja baada ya kuzindua Kikao kazi cha Wadau wa TASAF Mkoa wa Shinyanga waliofika katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga kushiriki uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya utoaji ruzuku na TASAF kwa kaya masikini.

Watekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF wataendelea kufanya kazi mkoani Shinyanga kwa kuwatambua wanufaika wa ruzuku za kaya masikini chini ya mpango wa TASAF kwa kutumia madiwani na watendaji wa vijiji pamoja na watendaji wa serikali kwa kuwabaini wale wote watakaonufaika na mradi huo kwa kutumia vigezo vilivyowekwa.

Post a Comment

0 Comments