Katibu UWT Longido: Mama Mdude ongea na mwanao, hatuwezi kuvumilia watu wanaomchafua Rais Samia

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Longido mkoani Arusha umekemea vikali baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakitumika vibaya kumkejeli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan huku wakitumia maneno ya dharau.
Kutokana na hali hiyo umoja huo wameanzisha kauli ijulikanayo kama "Mama Ongea na Mwanao" huku wakimsihi Rais kusonga mbele kwa kuchapa kazi na asiwasikilize hao.
Katibu wa UWT wilayani Longido, Judith Laizer ameyasema hayo wakati akizungumzia kuhusiana na siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

"Sisi Umoja wa Wanawake wa CCM Wilaya ya Longido tunakuomba popote ulipo mama mzazi wa kijana Mdude (kada wa CHADEMA, Mdude Nyagali) kuzungumza na mwanao ambaye ametoka gerezani hivi karibuni na kuanza kumshambulia mama Rais Samia Suluhu Hassan kwa maneno ya kejeli, zungumza nae aache mara moja,"amesema Laizer.

"Akumbuke kuwa alipokuwa gerezani waliokuwa wanaumia ni mama yake na ndugu zake hivyo sisi UWT Longido tunakuonya uache mara moja kutoa hoja za njaa za kumshambulia Rais wetu, tunaimani kupitia kauli ya mama yako mzazi utamheshimu pia,"amesema Laizer.

Pia akizungumzia wanaomdai Rais katiba mpya alisema kuwa, wamuache Rais afanye kazi kwa amani na utulivu kwani katiba ipo na inatosha.

Amesema kwamba, wanapaswa kusoma katiba iliyopo na kuielewa vipengele vyake na sheria zilizomo na kuridhika navyo.

Pia aliwataka kuheshimu mamlaka iliyopo ili kuifanya nchi kufika mahali inapotakiwa na kwa vijana ambao hawana mapenzi mema na nchi wanapaswa kukaa nao mbali.

"Hatutakubali kuona ndoto yako Rais Samia Suluhu Hassan inakatishwa na watu wachache wasio na mapenzi mema au chama chochote tutazidi kukuombea bila kujali kabila wala dini,"amesema.

Wakati huo huo katika kutimiza siku 100 ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Umoja wa Wanawake Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT) Wilaya ya Longido mkoani Arusha wamempongeza kwa uchapakazi kwa weledi mkubwa.

Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa umoja huo Wilaya ya Longido, Judith Laizer. Judith amesema kuwa, katika siku 100 za Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umekuwa na tija kwa jamii ukilinganisha na siku zenyewe kuwa chache kwani amekuwa halali,ameendelea kuweka uchumi vizuri huku akizindua miradi mbalimbali.
"Sisi Umoja wa Wanawake Wilaya ya Longido tunakupongeza sana mama kwa uchapakazi wako tukutie moyo usiogope, songa mbele tuko nyuma yako hata wanaume wako pamoja na wewe,"alisema Judith.

Aidha, amesema wao kama wanawake wa pembezoni hasa Wilaya ya Longido wamefurahishwa na utendaji kazi kwa kutumia ukarimu, upendo na weledi mkubwa bila ubaguzi na kwamba wataendelea kutangaza kazi nzuri anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment

0 Comments