MAKAMBA AAHIDI BARABARA, MAJI NA UMEME, ACHANGIA MILIONI MOJA UJENZI WA ZAHANATI

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba amesema Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi huduma ya barabara za vijijini, umeme na maji ili kuweza kurahisisha maisha yao.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba akiweka jiwe la msingi ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nkamai, Kata ya Mponde. Makamba alichangia fedha yake ya mfukoni sh. milioni moja ili kuchana mbao kwa ajili ya upauaji. (Picha na Yusuph Mussa).

Amesema haiwezekani Serikali kujinasibu kuwa inajenga barabara za maghorofa mijini, huku wakulima vijijini mazao yao yanaoza ama yananunuliwa kwa bei ya chini kutokana na barabara kuwa mbovu.

Akizungumza Julai 29, 2021 kwenye Kijiji cha Nkamai, Kata ya Mponde, Tarafa ya Soni katika Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Zahanati ya Nkamai, Makamba alisema hadi mwaka 2025, barabara za vijijini zitakuwa na uwezo wa kupitika mwaka mzima.

"Barabara za Jimbo la Bumbuli zinajengwa sasa hivi kama mkakati wa kuwasaidia wakulima kuweza kufanya shughuli zao ikiwemo kupeleka mazao yao sokoni, wananchi kusafiri ili kufanya biashara na huduma nyingine. Haiwezekani Serikali kusema kuwa imejenga barabara za juu au za maghorofa mijini, huku wakulima barabara zao zikiwa hazipitiki, huku wakishindwa kusafirisha mazao yao.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kulia) akimkabidhi sh. milioni moja Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkamai Paul Manase (kushoto) ili zitumike kuchana mbao kwa ajili ya upauaji wa zahanati ya kijiji hicho. (Picha na Yusuph Mussa).

"Ni lazima tukapiganie bungeni kuona barabara za vijijini zinajengwa kwa kiwango cha kuridhisha kwa kiwango cha changarawe na lami . Haiwezekani barabara za mijini zinajengwa njia nne, na zinakuwa pana kama uwanja wa mpira wa miguu, wakati huku vijijini wakati mwingine hawahitaji lami wala barabara ya ghorofa, bali wanachohitaji wao ni barsbara ipitike tu ili apeleke mazao yake sokoni," alisema Makamba.

Makamba alisema Jimbo la Bumbuli limepata sh. bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na kile cha changarawe, ambapo katika Mji wa Bumbuli wanakusudia kujenga barabara ya kilomita moja kwa kiwango cha lami ambayo imetengewa sh. milioni 500, huku barabara za kiwango cha changarawe kimetengewa sh. bilioni moja.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (wa pili kushoto) akiweka jiwe la msingi ujenzi wa maabara Shule ya Sekondari Chai, Kata ya Mponde. Kulia ni Diwani wa Kata ya Mponde Richard Mbughuni, na kushoto ni Katibu wa Mbunge ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwamkomole Hozza Mandia. (Picha na Yusuph Mussa).

Barabara za kiwango cha changarawe ni kutoka Bumbuli- Mayo kilomita zitakazofanyiwa matengenezo ni kumi, barabara ya Vuga- Mponde- Wena kilomita 21.2, barabara ya Balangai- Tamota- Vulii kilomita 13.7, barabara ya Vulii- Mahezangulu- Magoma kilomita 15.4, barabara ya Mbelei- Baga- Mgwashi- Nkongoi kilomita 28.8 na Soni- Mponde kilomita 13.4.

Lakini Jimbo la Bumbuli pia litanufaika na barabara ya kutoka Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano- Mashewa ya kilomita 70, huku ikiwa imetengewa sh. biluoni 3.5, kwani barabara hiyo itapita kwenye jimbo hilo kwenye Kata za Milingano na Kwamkomole.
Wananchi wa Kijiji cha Nkamai, Kata ya Mponde, wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nkamai inayoonekana kulia. Makamba alichangia fedha yake ya mfukoni sh. milioni moja ili kuchana mbao kwa ajili ya upauaji. (Picha na Yusuph Mussa).

Makamba alisema kwenye suala maji jitihada zinafanyika, ambapo kuna mradi mkubwa wa maji ambao utanufaisha kata yote ya Mponde, huku akisema pamoja na Kijiji cha Kweminyasa ndiyo pekee kimepata umeme kwenye kata hiyo, lakini tayari vijiji vyote vilivyobakia vipo kwenye mpango wa kupata umeme.

Akisoma risala, Mtendaji wa Kijiji cha Nkamai Paul Manase alisema katika zahanati hiyo ambayo ipo kwenye hatua ya kupaua, imetumia sh. milioni 13,870,000, ambapo kati ya fedha hizo, sh. milioni 3,870,000 ni fedha za Mfuko wa Jimbo, na zilizobaki ni nguvu za wananchi. Na kukamilisha ujenzi, kunahitajika sh. milioni 3,582,000.

Katika kuona zahanati hiyo ambayo imepewa jina la Zahanati ya January Makamba, yeye Makamba alitoa fedha zake za mfukoni sh. milioni moja ili kuchana mbao kwa ajili ya upauaji.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kushoto) akiangalia ujenzi wa miundombinu ya maabara Shule ya Sekondari Chai, Kata ya Mponde. (Picha na Yusuph Mussa).

Akiwa Shule ya Sekondari Chai, iliyopo Kata ya Mponde, pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye maabara ya shule hiyo ambayo Serikali ilitoa sh. milioni 30 kwa ajili ya umaliziaji, Makamba pia ametoa bati 30 kwa ajili ya umaliziaji chumba cha darasa, huku akiwanusuru wanafunzi wa kidato cha kwanza wasisome kwenye vumbi baada ya kuagiza darasa hilo leo Julai 30, 2021 liwekwe sakafu, ambapo ametoa fedha zake mifuko ya saruji 15 na lori la mchanga kwa kazi hiyo vyenye thamani ya sh. 475,000.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Zeba darasa la sita katika Kijiji cha Zeba, Kata ya Mponde, Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wakiwa darasani huku wamevaa barakoa kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona. Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani January Makamba alifika hapo Julai 29, 2021 kukagua miradi ya maendeleo. (Picha na Yusuph Mussa).

Kwenye Shule ya Msingi Zeba iliyopo Kata ya Mponde, ambapo pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa darasa ambao umefikia zaidi ya asilimia 90, ameahidi wiki ijayo kupata umeme kama ilivyokuwa Shule ya Sekondari Chai, ambao nao watapata umeme wiki ijayo. Pia ametoa bati 20 kwa fedha zake ili kuweka bati jipya Ofisi ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Zeba, huku akiahidi shule hiyo kufanyiwa ukarabati mkubwa wa vyumba vya madarasa, ukiwa ni mpango wa Serikali kukarabati shule kongwe.

Diwani wa Kata ya Mponde Richard Mbughuni alimueleza Makamba kuwa kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara, umeme, maji, uchimbaji wa madini usio na tija ambao unaharibu mazingira na ukosefu wa chakula cha mchana kwenye baadhi ya shule.

Post a Comment

0 Comments