Mti alioutumia Mwalimu Nyerere kupanda juu kuokoa maisha yake wakati akitafutwa na Mkoloni waibu mjadala

NA FRESHA KINASA

Umoja wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bunda mkoani Mara pamoja na wananchi wameiomba Serikali iweze kuyatambua maeneo matatu ya kihistoria yaliyosahaulika aliyoyatumia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Mwitongo Butiama , Emmanuel Kiondo akieleza jambo kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bunda, Magwa Malala mwenye suti ya kijani, pembeni yake ni kiongozi wa chama hicho ngazi ya kata na mwenye shati jeupe ni Madaraka Nyerere. (Picha na Diramakini Blog).

Eneo la Masaba lililopo Kata ya Salama wilayani Bunda ni miongoni mwa maeneo hayo ambalo lina miti mitano na miongoni mwa miti hiyo, mmoja wapo Mwalimu Nyerere alipanda juu kuokoa maisha yake wakati akitafutwa na Mkoloni.

Pia nyumba aliyotumia kufanya vikao vya siri na machifu iliyopo eneo la Ikizu Misheni Wilaya ya Butiama pamoja na pango alilokaa wakati akiandika Katiba ya TANU lililopo Kijiji cha Makongoro wilayani humo.

Rai hiyo wameitoa wakati wa ziara maalumu ya kutembelea maeneo hayo iliyowahusisha familia ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiongozwa na Chifu Japheti Wanzagi, Mtoto wa Baba wa Taifa Madaraka Nyerere, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Baba wa Taifa yaliyopo Mwitongo Butiama, Emmanuel Kiondo pamoja na viongozia wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Bunda.

Viongozi hao walifanikiwa kuyatembelea maeneo hayo huku wananchi pia wakihimiza yatambulike na kuhifadhiwa kama historia na kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Nchagwe Bita akisoma historia ya eneo la Masaba kwa niaba ya umoja wa chama hicho katika Kijiji cha Masaba ulipofanyika mkutano ambapo kuna miti mitano mikubwa tangu enzi za ukoloni amesema, eneo hilo lina miti ambapo kati ya miti hiyo Mwalimu Nyerere alipanda juu kujificha wakati akiwa njiani kwenda kwa rafiki yake kwa mzee Kiberiti Mias Nyamoko.

Ni baada ya kugundua anafuatiliwa nyuma na gari la Mkoloni, kwani alikuwa akienda kukutana na machifu kufanya kikao cha siri nyakati za usiku kwa lengo kutafuta uhuru wa Tanganyika.

"Zamani likiitwa eneo la Imalelo limekuwepo kabla ya Uhuru mwaka 1956 Mwalimu akiwa anakwenda kukutana na machifu na kuhamasisha wananchi kujiunga na TANU alipofika eneo hilo aligundua anafuatiliwa na mkoloni nyuma na ndipo alipomwambia dereva wake amteremshe, Mwalimu alipanda juu ya mti mmoja wapo na muda mfupi gari la mkoloni lilipita na lilipo mpata dereva wa Mwalimu, Mwalimu hakuwa ndani ya lile gari.

Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Chifu Japhet Wanzagi (aliyesimama) akieleza jambo,  kulia kwake ni Madaraka Nyerere na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Bunda, Magwa Malala wakiwa katika kikao na wananchi wa Kijiji cha Masaba Kata ya Salama Wilaya ya Bunda walipotembelea maeneo ya kihistoria yaliyosahaulika ambayo Mwalimu Nyerere aliyatumia katika harakati zake za kutafuta Uhuru wa Tanganyika. (Picha na Diramakini Blog).

"Mwalimu aliteremka juu ya mti na kubadili njia akatembea kwa mguu umbali wa kilomita 19 kupitia njia ya Salama Kati, Nyameka na kufika Bukama kwa rafiki yake Kiberiti Mias Nyamoko-Bukama kuendelea na kazi yake,"amesema.

Ameongeza kuwa, eneo hilo limeachwa wazi kwa muda mrefu likiwa na miti hiyo huku likipewa heshima kubwa na kuenziwa kutokana na kuokoa maisha ya Baba wa Taifa.

Pia aliongeza kuwa,eneo hilo halitambuliki kutokana na barabara ya kufika katika eneo hilo kutopitika hususan nyakati za mvua, na pia eneo hilo halijawekewa alama yoyote kutambulisha kwamba ni Makumbusho ambapo amesema hali hiyo inaweza kupelekea kupotea kwa kumbukumbu hiyo muhimu, na hivyo jitihada thabiti za makusudi zinahitajika.

Aidha, aliomba katika eneo hilo Serikali ijenge chuo Cha VETA kama ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa, pia kujengwa kwa lami barabara ya Buhemba-Nyaburundu, Kurusanga, Rakana hadi Mgeta kama ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa pamoja na barabara ya Kurusanga, Salama Kati hadi Bukama kwani maeneo hayo yote Mwalimu alikuwa akipita akiwa katika harakati zake za kutafuta Uhuru wa Tanganyika ambao hata hivyo, ulipatikana bila kumwaga damu kutokana na mikakati thabiti ya Mwalimu Nyerere.

Naye Chifu kutoka Ukoo wa Burito ambaye pia ni Msemaji wa familia ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere Japhet Wanzangi aliwapongeza wananchi wa kijiji hicho kulienzi eneo hilo kwani liliokoa uhai wake, amesema ukanda huo Mwalimu alikuwa na marafiki wengi ambao kwa namna moja ama nyingine walimtia moyo katika harakati zake za kudai Uhuru akiwemo Chifu Makongoro na Mzee Kiberiti Miasi Nyamoko alikuwa anaishi Kijiji cha Bukama.

"Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa juhudi zote, tusipofanya hivyo tutakuwa kama Mtume Paulo alivyowaambia Wagalatia 'Nani kawaloga' mchango wa Mwalimu Nyerere ni mkubwa sana kwa Taifa letu kwa hiyo vijana lazima warithishwe na kufundishwa yote ambayo Mwalimu aliyaishi, niwapongeze pia wananchi kwa kutunza miti hii bila kuikata imekuwepo tangu nchi haijapata Uhuru,"amesema Chifu Wanzagi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Bunda Vijijini, Magwa Malala amesema kuwa, lengo la ziara hiyo ilikuwa kukusanya historia ya maeneo ya Baba wa Taifa yaliyosahaulika yaweze kutambulika kwani yakitambulika yatatumika kutoa fundisho jinsi Mwalimu alivyojitoa sadaka kupigania uhuru usiku na mchana hadi kufanikisha azma yake na kwa sasa wananchi wanafurahia matunda ya Uhuru.

Amewataka Watanzania kuthamini kwa dhati mchango mkubwa uliofanywa na Mwalimu Nyerere hususan kuliletea Uhuru Taifa, ambapo misukosuko mingi na mizito aliipitia usiku na mchana kutokana na Mkoloni kutokuwa tayari kumuona akijishughulisha na harakati za kudai uhuru na hivyo alifuatiliwa kila kona ingawa hawakuweza kudhibiti nia iliyokuwa ndani mwake.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyopo Mwitongo Wilaya ya Butiama amesema kuwa,uwepo wa maeneo hayo ni baraka, heshima na utajiri mkubwa wa kihistori na ni muhimu sana kwa kizazi cha sasa na kijacho kujifunza.

Amesema, baada ya kuyatembelea na kuyaona utafanyika utaratibu wa kuyaendeleza kwani hata yeye alikuwa akisikia, lakini baada ya kufika na kujionea alisema yataingizwa katika historia.

Pia, Kiondo amewaomba Watanzania kuendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwitongo ili kujifunza mambo mbalimbali aliyoyafanya Mwalimu enzi za uhai wake pamoja na kujionea zawadi mbalimbali alizopewa na mataifa ya nje kutokana na kutoa mchango kuyasaidia ikiwemo kupata Uhuru na kujifunza yale ambayo Mwalimu aliyaishi ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kurithishwa maarifa kutoka katika Makumbusho hayo.

Samwelly Kiberiti ambaye ni mtoto wa Mzee Kiberiti Mias amesema, mwaka 1952 Mwalimu Nyerere alifika katika nyumba ya Baba yake Kiberiti Miaz na baadaye aliendelea kuwa akifika katika familia yao na nyakati za usiku machifu walijumuika kwa pamoja kufanya vikao nyakati za usiku ambapo mikakati mbalimbali ilifanyika kwa siri Mkoloni asitambue.

Huku akisisitiza kuwa, pia Mwalimu wakati mwingine alilala katika nyumba ya baba yake mzee Kiberiti ambaye licha ya kutojua kusoma na kuandika, lakini Mwalimu alimthamini na kumpenda.

Mahunda Kiberiti mtoto wa Mzee Kiberiti alizaliwa mwaka 1945 amesema, kulikuwa na urafiki mkubwa kati ya Mwalimu Nyerere na Mzee Kiberiti na urafiki huo ulianzishwa na chifu Makongoro ambaye pia alikuwa chifu wa kabila la Waikizu.

Amesema, Mwalimu alikuwa akifika kwa mzee Kiberiti na machifu kutoka sehemu mbalimbali walijumuika na walikaa ndani usiku kufanya mazungumzo juu ya kupata Uhuru wa Tanganyika. Huku akisema urafiki huo ulidumu hadi Mwalimu Nyerere alipofariki dunia.

"Baada ya Uhuru taifa lilikuwa zuri sana, baba yangu Mzee Kiberiti alishikamana sana na Mwalimu Nyerere na Chifu Makongoro na machifu wengine walikuwa wamoja kuhakikisha taifa linapata Uhuru. Naomba Watanzania tumuenzi kwa vitendo kwa kuleta Uhuru wa nchi yetu, na pia nyumba hii ambayo Mwalimu alifanyia vikao vya kutafuta uhuru na wenzake watusaidie kuikarabati na kuiboresha kipindi kile ndio ilikuwa nyumba kubwa maeneo haya,"amesema Mahunda Kiberiti.

Seleman Makongoro ni Mtoto wa Chifu Makongoro ambaye pia alikuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere amesema kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa akifika katika familia yao na baadaye aliteremka hadi eneo la pango ambapo aliingia na kukaa humo kwa kazi ya kuandika katiba ya TANU.

Amesema kwamba, mtu yeyote asingetambua kwamba mwalimu yupo eneo hilo kwani hata Mkoloni alikuwa hafiki. Aliiomba serikali kuyatambua maeneo hayo kwani yana umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news