Mwalimu Makuru afichua siri utendaji mbovu unavyoumiza Taifa kupitia miradi

Na Amos Lufungilo,Musoma

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema kuwa,changamoto ya utendaji kazi na usimamizi mbovu wa miradi ya Serikali unaofanywa na baadhi ya watendaji unachangia kuligharimu Taifa fedha nyingi.

Mwalimu Makuru ameyasema hayo kupitia mahojiano maalum aliyoyafanya na DIRAMAKINI Blog mjini Musoma ambapo amewataka watendaji wote wanaoaminiwa na Serikali kwa ajili ya kusimamia miradi yake kuzingatia weledi, nidhamu na kutanguliza mbele maslahi ya umma.

"Tuache tabia ya ubinafsi na udokozi ambayo imekuwa ikichangia Taifa kupoteza mabilioni ya fedha kutokana na tamaa za baadhi ya watendaji ambao wanaaminiwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo nchini, tutangulize uzalendo na maslahi ya Taifa mbele ili kuipa thamani na hadhi miradi yote iweze kudumu na kuwa na tija kwa umma,"Mwalimu Makuru ameieleza DIRAMAKINI Blog katika mahojiano.

Mwalimu Makuru ameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na mingine ambayo inatumia fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi, mikopo au misaada kutoka kwa wahisani, hivyo watendaji wanapokosa uaminifu na kuanza kujipa wao kipaumbele kupitia miradi hiyo, hali hiyo inachangia Taifa kuzidi kupoteza fedha.

"Watambue kuwa, Serikali inatoa fedha nyingi ili kutekeleza miradi ambayo itasaidia kuharakisha maendeleo iwe mijini au vijijini, sasa inapotokea watu wanatumia nafasi zao kutumia njia za mkato ili waweze kupata chochote kitu wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, wajue kuwa wanasababisha hasara kubwa kwa Serikali na pia wanasababisha maumivu kwa wananchi maana fedha zinazovujishwa zinatokana na kodi zao,"amesema Mwalimu Makuru.

Amesema, amekuwa akisikitishwa na miradi ambayo imekuwa ikijengwa chini ya kiwango ambayo haiendani na fedha iliyotengwa na serikali, hivyo kuharibika kabla ya wakati na wakati mwingine ikishindikana kutumika kwa kuhofia kuhatarisha usalama wa wananchi.

"Kiukweli inasikitisha sana pale ambapo serikali inatoa fedha nyingi katika miradi yake ya kimaendeleo kwa wananchi na viongozi waliopewa dhamana kushindwa kusimamia kwa dhati na kwa weledi, hivyo kujikuta taifa linaingia hasara kubwa kwa kupoteza pesa nyingi ambazo ni za walipa kodi wa Tanzania na zingine ni misaada toka nje ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikitolewa kwa ajili ya kujenga miradi ya kiuchumi na kijamii, ila pamekuwepo na usimamizi dhaifu kwa baadhi ya viongozi ambao umekuwa hauna tija,"ameongeza.

Mwalimu Makuru amesema kuwa,kipindi mbio za Mwenge wa Uhuru zilipokuwa Mkoa wa Mara baadhi ya miradi katika wilaya za mkoa huo ilibainika ipo chini ya kiwango wakati wa uzinduzi au kufunguliwa, hivyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge akatoa maelekezo.

Alisisitiza kwa kusema, hata kiongozi wa kitaifa wa mbio za Mwenge alisema hata baadhi ya miradi iliyojengwa ndani ya mkoa wa Mara haikuendana na thamani ya pesa zilizotumika katika ujenzi wa miradi hiyo hususani Wilaya ya Serengeti na wilaya zingine ndani ya mkoa wa Mara.

Mwalimu Makuru amesema, kutokana na miradi mingi ya serikali ndani ya mkoa wa Mara kuwa dhaifu na chini ya kiwango ni kutokana na usimamizi wa viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya usimamizi kushindwa kuwa wazalendo,hivyo tamaa zao kuligharimu taifa.

Mwalimu Makuru amewasihi viongozi waliopewa dhamana ya usimamizi wa miradi ya wananchi ya kimaendeleo waweke mbele uzalendo na wafanye kazi kwa bidii na kwa haki pasipo kumpendelea mtu yeyote yule au mkandandarasi yeyote yule.

"Maana bila usimamizi thabiti wa miradi ya serikali nchini, serikali itakuwa inapata hasara kubwa sana,"amesema Mwalimu Makuru.

Pia Mwalimu Makuru amezidi kubainisha kwamba, miradi mingi ambayo kiongozi wa mbio za mwenge ameifikia na kuona kuna mapungufu, wataalamu wa Serikali waifuatilie miradi hiyo kwa kina ili kubaini kama kuna uzembe wa viongozi au wasimamizi wazembe wafuatiliwe na kuwajibishwa ili kuleta nidhamu na uwajibikaji katika taifa na kuongeza imani kwa wananchi juu ya viongozi wao na serikali.

Wakati huo huo, Mwalimu Makuru ameiomba Serikali kuendelea kuwa na ufuatiliaji mkali kwa baadhi ya makandarasi na mafundi ambao wamekuwa wakifanya kazi za miradi ya serikali chini ya kiwango kwa kushirikiana na viongozi waliopewa dhamana ya usimamizi wa miradi ya serikali hapa nchini.

Pia Mwalimu Makuru amempongeza, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kutoa pesa nyingi katika miradi mingi hapa nchini.

Mwalimu Makuru amemuomba, Mheshimiwa Rais Samia kuongeza pesa katika miradi ya kiuchumi ya kimaendeleo hususani katika miundombinu ya barabara kama vile barabara ya Musoma kuelekea Serengeti, Musoma Busekera,Tarime Serengeti kupitia Nyamongo kwani itarahisisha maendeleo ya kiuchumi ya wananchi ndani ya mkoa wa Mara endapo itamalizika kwa wakati kutekelezwa.

Post a Comment

0 Comments