NAIBU WAZIRI MABULA AAGIZA MASHAURI YA ARDHI KUISHA NDANI YA MIAKA MIWILI

Na Munir Shemweta, MBARALI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maenseleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amewaagiza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu shauri kufunguliwa.

Dkt.Mabula alitoa agizo hilo tarehe 16 Julai 2021 wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakati akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbarali mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya tarehe 16 Julai 2021. wa pili kushoto ni mkuu wa wilaya ya Mbarali Reuben Mfune na wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tullo.

Naibu Waziri wa Ardhi aliwaagiza pia wenyeviti na watumishi katika Mabaraza ya Ardhi kuhakikisha wanatumia uzoefu wao kuelimisha wananchi kuhusu taratibu muhimu zinazopaswa kuzingatiwa katika uendeshaji wa mashauri yatokanayo na migogoro ya ardhi kuwarahisishia wanaofuatilia haki zao.

“Ninawaagiza Wenyeviti na watumishi katika mabaraza kuhakikisha mnatumia uzoefu wenu kuwaelimisha wananchi taratibu muhimu katika uendeshaji mashauri kuwarahisishia wanapofuatilia mashauri yao,” alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa vyombo vya kushughulikia migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi inalo jukumu la kuvipatia vitendea kazi vyombo hivyo ili viweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mbarali mkoani Mbeya wakati wa uzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mbarali tarehe 16 Julai 2021.

Alisema, wizara yake itaendelea kuyapatia vitendea kazi Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya ili kuhakikisha Mabaraza hayo yanatoa huduma ya kutatua migogoro ya ardhi kwa urahisi.

Alitoa rai kwa halmashauri zote nchini kuhuisha Mabaraza ya Kata na Vijiji kwa yale yaliyomaliza muda wake na kutoa elimu kwa wajumbe wake ili kufahamu majukumu yao.

“Halmashauri nyingi hazitengi bajeti kwa ajili ya kuwawezesha wajumbe kupata vitendea kazi kama vile shajala na usafiri jambo linalofanya mabaraza ya kata na vijiji kujiamulia kuweka tozo kwa wananchi bila kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa Mabaraza,” alisema Dkt. Mabula.  
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akikagua ofisi ya Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya mara baada ya kulizindua tarehe 16 Julai 2021.

Aliwataka wajumbe walioteuliwa kufanya kazi kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kufanya kazi kwa weledi na kuepuka vishawishi vya rushwa ili kujenga imani kwa wananchi.

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya Stela Tulo aliupongeza uongozi wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kwa juhudi zake zilizowezesha uanzishwaji baraza hilo.  
Msajli wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tullo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya tarehe 16 Julai 2021.

Aliwataka wananchi wa Mbarali kulitumia vizuri baraza hilo la Ardhi na kuongeza kuwa, Wizara ya Ardhi imejipanga kuhakikisha inaanzisha mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya katika wilaya nyingine ili kuweza kutatua migogoro ya ardhi iliyoshindikana kwa njia ya mazungumzo.

Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mbarali linafanya mkoa wa Mbeya kuwa na jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya matatu. Mabaraza mengine ni yale ya wilaya za Tukuyu pamoja na Kyela.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula akimkabidhi hati za umiliki wa ardhi kwa Katibu wa CCM wilaya ya Mbarali Abdalaah Mpokwa wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mbarali tarehe 16 Julai 2021. Kulia ni Kamishna wa Ardhi nchini Methew Nhonge.

Aidha, Naibu Waziri Mabula mbali na uzinduzi wa Baraza la Ardhi aligawa hati za ardhi 144 kwa wamiliki wa ardhi katika wilaya ya Mbarali waliorasimishiwa makazi yao na kuwaeleza kuwa hati walizokabidhiwa zitawahakikishia usalama wa miliki zao pamoja na kuzitumia katika shughuli za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news