Rais Dkt.Mwinyi afanya mazungumzo na Balozi mdogo wa Oman

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake wa kihistoria kati yake na Oman ikiwa ni pamoja na kushirikiana kibiashara, kiuchumi na kijamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Balozi Mdogo wa Oman anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe. Said Salim Al Sinawi, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar, Said Salim Alsinawi ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amemkaribisha Zanzibar Balozi Alsinawi na kumuhakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wote wataendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman ambao ni wa kihistoria.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amemuhakikishia Balozi huyo mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman kwani inathamini sana juhudi za Ubalozi huo za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Oman na inatambua hatua na juhudi mbalimbali inazozichukua Serikali ya Oman katika kuiunga mkono Zanzibar hivi sasa ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa Jumba la Beit Al Jaib pamoja na Jumba la Wananchi “Peoples Palace”, lililopo Forodhani

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, ujenzi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar huku akisisitiza kwamba kuna kila sababu ya kuzitunza nyumba za Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na haiba yake.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi amemueleza Balozi huyo kwamba uwepo wa Kampuni ya ndege ya Oman Air yenye kufanya safari kati ya Zanzibar na Oman kumeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha biashara kati ya pande mbili hizo huku akisisitiza kwamba Zanzibar ina bidhaa nyingi zenye soko nchini Oman.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi Mdogo wa Oman anayefanyia Kazi zake Zanzibar Mhe.Said Salim Al Sinawi, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha rasmin leo 13-7-2021.(Picha na Ikulu).

Mapema, Balozi Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar, Said Salim Alsinawi alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba Serikali ya Oman ipo tayari kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono katika kumarisha miradi yake ya maendeleo.

Balozi huyo Mdogo wa Oman amemueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba, Serikali ya Oman inatambua uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya Oman na Zanzibar pamoja na watu wake hivyo, nchi yake itaimarisha zaidi mahusiano yaliopo.

Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa Oman inathamini uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo na inatambua juhudi kubwa anazozichukua Rais Dk. Mwinyi za kuiletea Zanzibar maendeleo hivyo haina budi kumuunga mkono ili kufikia lengo lake alilolikusudia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news