Rais Dkt.Mwinyi: Imarisheni Sera ya Diplomasia ya Uchumi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuiimarisha Sera ya Diplomasia ya Uchumi ili Zanzibar nayo iweze kupata fursa zaidi katika kuimarisha uchumi wake.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 29, 2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wake Balozi Liberata Rutageruka Mulamula.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, uchumi wa Zanzibar unategemea sana kazi zitakazofanywa na mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina bidhaa nyingi za kuuza nje ya nchi zikiwemo viungo.

Ameeleza kwamba, kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikiingiza bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi na kutokuwa na bidhaa nyingi ambazo zinazotoka Zanzibar na kuweza kuuzwa nje ya nchi.

Hivyo, Rais Dkt. Miwnyi amesisitiza haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuiimarisha Sera ya Diplomasia ya Uchumi ili iweze kuleta tija zaidi hasa kwa upande wa Zanzibar kwa azma ya kuweza kupata soko kwa bidhaa zake inazozalisha.

Amesema kuwa, kuna nchi kadhaa zikiwemo zile za Jumuiya ya Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Oman na nchi nyinginezo zinahitaji bidhaa za Zanzibar, hivyo juhudi za makusudi zikichukuliwa mafanikio yanaweza kupatikana katika nyanja hiyo hasa ikizingatiwa kwamba fursa ipo.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja ya kutilia mkazo suala zima la kuunganishwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar na wale wa nje ya nchi zikiwemo nchi hizo za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE) na nyinginezo.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alitoa shukurani kwa uongozi wa wizara hiyo ukiongozwa na Waziri wake Balozi Mulamula kwa kuja Ikulu kujitambulisha kwake na kueleza kwamba utaratibu wa kukutana mara kwa mara ni mzuri kwani unajenga zaidi mahusiano.

Rais Dkt. Mwinyi pia, alipongeza hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo katika kuziweka katika mazingira mazuri ofisi za wizara hiyo zilizopo hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, akieleza suala zima la Diaspora, Rais Dkt.Mwinyi alisisitiza haja ya Wanadiaspora kuangaliwa uwezekano wa kuanza kupewa baadhi ya haki za raia za nchini mwao ili waweze kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo nchini mwao zikiwemo zile za uwekezaji huku hatua nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi aliueleza uongozi huo mwelekeo na Sera ya Zanzibar katika kujikita na uchumi wa Buluu hiyo ni kutokana na mazingira ya Zanzibar ambayo visiwa vyake vimezungukwa na bahari.

Mapema Balozi Liberata Rutageruka Mulamula alimueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya uongozi wa wizara hiyo kuja kujitambulisha kwake sambamba na kuja kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kishindo.

Balozi Mulamula alieleza lengo kuu la wizara yake ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akitoa shukurani za dhati kwa ushirikiano mzuri inayopata wizara hiyo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uamuzi wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imeleta mafanikio makubwa na imekuwa msaada mkubwa kwa wizara yake katika kutekeleza majukumu yao.

Balozi Mulamula alisema kuwa, kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar kumeweza kuwavutia watu wengi ambao wameonesha nia ya kuja kufanya kazi hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Balozi Mulamula alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa teuzi zake anazozifanya na alizozifanya ambazo zimekuwa zikizingatia jinsia.

Katika mazungumzo hayo pia, Balozi Mulamula alieleza kwamba ofisi za wizara yake zilizopo Zanzibar zimekuwa zikifanya kazi vizuri na kuweza kutoa ushirikiano mzuri kwa Serikali.

Kwa upande wa Diaspora, Waziri Mulamula alieleza azma ya wizara hiyo katika kuhakikisha inalipa kipaumbele suala la Wanadiaspora hasa ikizingatiwa hivi sasa wizara yake inaipitia Sera yake ya mwaka 2001.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news