Rais Dkt.Mwinyi: Nandy Festival ni fursa ya kuutangaza utalii wa Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Tamasha la “Nandy Festival” na kusema kwamba kufanyika kwa Tamasha hilo hapa nchini ni fursa ya kuutangaza utalii wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza na wasanii wa Tamasha la “Nandy Festival” waliopo hapa Zanzibar wakiongozwa na mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliupongeza utayari wa wasanii wa tamasha la “Nany Festival” kwa kuja Zanzibar na kufanya maonyesho hatua ambayo alisema ni faraja kwani maonyesho hayo yataendelea kuitangaza zaidi Zanzibar.

Alieleza jinsi alivyofurahishwa na na hatua hiyo na kueleza kwamba ataendelea kushirikiana na wasanii hao na kila itakapowezekana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa msaada utakaohitajikwa kwa lengo la kuitangaza Zanzibar na kuinua vipaji vya wasanii wake hasa ingazingatiwa kwamba tayari wasanii wa Tanzania Bara wamepiga hatua kubwa katika tasnia hiyo ya muziki.
Msanii wa Muziki wa Bongo Fleva Faustina Charles ( Nandy ) akizungumza wakati walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, akiwa Zanzibar katika onesho lake la Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21-7-2021 katika Uwanja wa Mao Zedung Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa licha ya kuwepo kwa matamasha mengi hapa Zanzibar lakini pia kufanyika kwa matamasha kama hayo ya “Nandy Festival” ni fursa ya kuyaendeleza matamasha kwani lengo ni kuwa na matamasha mengi ambapo ndani ya miezi yote 12 kukawepo matamasha na baada ya hapo kila mwezi ni vyema yawepo hata matamasha mawili.

Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa matamasha yana umuhimu mkubwa sana kwa sababu yanaleta watu kutoka nje na kusema kwamba muziki wa kizazi kipya nao unaweza kuleta watu wengi hapa nchini.

Alisema kuwa muziki wa kizazi kipya unaweza kuleta wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania ambapo wageni wanaotakiwa Zanzibar si lazima watoke nje, kwani hata wageni wanaotoka katika maeneo ya ndani ya Tanzania ikiwemo Kigoma, Arusha, Mwanza pia ni wageni kwani nao watakuwa na manufaa ya kiuchumi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, wakiwa Zanzibar wakishiriki katika Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21/7/2021 katika Uwanja wa Mao Zeding.(Picha na Ikulu).

Alisisitiza kwamba ni vyema mashirikiano yakawepo kati ya wasanii hao na Serikali na kufanya matamasha mengi zaidi huku akisisitiza haja kwa Serikali kuwashika mkono wasanii sambamba na kushirikiana nao kikamilifu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba michezo nayo inaweza kuimarisha uchumi na kuutangaza utalii wa Zanzibar na kutolea mfano mashindano ya Marathon yaliyofanyika hivi karibuni hapa Zanzibar yatasaidia kuitangaza Zanzibar.

Kwa upande wa muziki wa taarab, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa muziki huo hapa Zanzibar ni nyumbani hivyo, ni vyema hatua za makusudi zikachukuliwa katika kuuinua muziki huo kwani hapo siku za nyuma uliimarika zaidi ambapo palikuwepo hata mashindanio ya taarabu yaliyohusisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hatua ambayo ilikuwa inanyanyua vipaji vya wasanii wa ndani na kuleta hamasa na kuinua utalii.

Hivyo, alisema kwamba wakati umefika wa kurudisha matamasha ya muziki wa taarab na kumtambulisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo ambae atakuwa kiungo katika kushughulikia masuala hayo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alieleza utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kushirikiana na wasanii hao kwani kama unavyopendwa muziki wa kizazi kipya pia na muziki wa taarabu nao umekuwa na wapenzi wengi hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva ukiongozwa na Mwanamuzi Nandy, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, wakiwa Zanzibar katika Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21/7/2021.Katika uwanja wa Mao Zedung Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Katika maelezo yake, Rais Dk. Miwnyi alisisitiza kwamba Serikali anayoiongoza itatumia njia ya kuwasaidia wasanii wa ndani ili waweze kuinua vipaji vyao.

Alisema kwamba sanaa ni njia moja wapo ya kutoa ajira kwa vijana na kusema kwamba iwapo wasanii hao watasaidiana na wasanii wa Zanzibar hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa ajira vijana.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi na shukurani kwa Nandy na wasanii wenzake kwa kufanya tamasha hapa Zanzibar na kukutana nao lei hii pamoja na hapo jana kukutana na mkewe Mama Mariam Mwinyi huku akitumia fursa hiyo kwa kumshukuru na kumpongeza Nandy na wasanii wengine kwa ushirikiano wao mkubwa katika Kampeni za uchaguzi za CCM zilizopita.

“Nyinyi wasanii wa muziki wa kiziazi kipya mna uwezo mubwa wa kuvuta watu kwa hiyo wakati wa kampeni milikuwepo nyinyi na kina Aisha na wasanii kadha wa kadhaa kwa kweli tuna deni kwenu na tungependa kushirikiana katika masuala ya ajira na kuutangaza utalii wa Zanzibar”,alisema Dk. Mwinyi.

Nae mwanamuziki nguli wa kizazi kipya hapa nchini Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba yeye na wasanii aliokuja nao kwa ajili ya Tamasha lake la “Nandy Festival”,wamepata mapokezi makubwa hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Alisema kuwa mbali ya kufanya tamasha hilo pia, wakiwa hapa Zanzibar walipata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Aidha, Nandy aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya kwa kuwa nao karibu tokea alipowasili yeye na wasanii wenzake hapa Zanzibar kwa ajili ya tamasha la “Nandy Festival”.

Alisema kuwa Tamasha la “Nandy Festival” lilianza mwaka 2019 na kuweza kuzunguka Tanzania nzima wakati huo na mwaka uliofuata hawakuweza kufanya hivyo kutokana na kuwepo kwa maradhi ya COVID 19, lakini mwaka huu wameweza kuendelea na tamasha lao hilo na walishatembelea mikoa ikiwemo Kigoma, Mwanza, Dodoma na Arusha na hivi sasa kupata nafasi ya kuja Zanzibar.

Aliongeza kuwa tamasha hilo limekuwa likisaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa vijana kuweza kupata ajira kutoka makundi kadhaa akisema kwamba lengo ni kukuza muziki wa kizazi kipya barani Afrika.

Nandy aliahidi kushirikiana na wasanii wa Zanzibar ili kuupeleka mbele muziki wa kizazi kipya huku akieleza kwamba ipo haja ya kushikwa mkono na Serikali katika kuhakikisha wanafanikisha zaidi matamasha yao.

Nae Meneja wa Nandy, Moko Biashara aliwasisitiza wasanii kupambana huku akiahidi kuisaidia Zanzibar katika kuitangaza kiutalii.

Muimbaji wa muziki wa taarab maarufu hapa nchini Isha Mashauzi nae wka uapnde wake alimueleza Rais Dk. Mwinyi umuhimu wa kufanyika kwa tamasha la “Taarab Festival”, hapa Zanzibar kama lilivyofanyika tamasha la “Nandy Festival”, kwa lengo la kuutangaza muziki huo na kuitangaza Zanzibar kwani ina vipaji vingi.

Mashauzi alieleza hamu yake ya kuja Zanzibar kushirikiana na wasanii wa hapa visiwani katika kuuendeleleza na kuutangaza muziki wa taarab huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuiongoza Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news