RC Gabriel aipongeza TARURA kwa kuanza kutumia Mfumo wa TeRMIS

Na Bebi Kapenya,TARURA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuanza kutumia mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya Kielektroniki ujulikanao kama “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) katika Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa kuutambulisha mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ujulikanao kama (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambao umeanza kutumika mkoani Mwanza.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kuutambulisha mfumo huo ambao umeanza kutumika rasmi mkoani Mwanza tarehe 20 Julai, 2021.

Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kuwa lengo la mfumo huo ni kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatakayosaidia maboresho na maendeleo ya miundombinu ya barabara kwani mfumo utampa fursa mtumiaji wa maegesho kulipia ushuru wa maegesho kwa saa, masaa, siku, wiki au mwezi, pia mfumo utatoza ushuru wa vyombo vya moto vilivyoegeshwa kwenye maeneo ya maegesho tu na si vinginevyo na pia mfumo utasaidia wateja kufanya maombi na kulipia huduma kwa njia ya mtandao bila kufika ofisi za TARURA.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza TARURA kuanza kutumia mfumo huu kwani utaleta tija katika ukusanyaji mapato ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi kwasababu malipo yatapokelewa serikalini moja kwa moja na malipo yote yatafanyika kwa kutumia kumbukumbu namba ya malipo”, amesema Mhandisi Gabriel.
Afisa Tehama kutoka TARURA Bw. John Malasa akitoa mafunzo ya mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) kwa wadau wa usafirishaji Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kuwaelimisha namna mfumo utakavyofanya kazi wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Mwanza.

Pia, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mtumiaji wa chombo cha moto akiegesha chombo kwenye maegesho atapatiwa kumbukumbu namba ya malipo, ambapo atatumia kumbukumbu namba hiyo kufanya malipo kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, matawi ya Benki au kupitia kwa Mawakala.

Aidha, Mhandisi Gabriel amewataka TARURA kuhakikisha elimu ya matumizi ya mfumo inafika kikamilifu kwa wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja lengo kikiwa ni kuepusha malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Pia, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kupokea mabadiliko hayo na kuanza kulipa wao wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (hayupo pichani) wakati wa kuutambulisha mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Mwanza.

Kwa upande wake Afisa Tehama wa TARURA, Bw. Shadrack Mahenge amesema mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato yaani “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Iringa, Singida, Dodoma na Mwanza na unatarajia kusambazwa nchi nzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news