Ripoti: Wahamiaji wa Kimataifa wameongezeka

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inakadiria kwamba kati ya mwaka 2017 na 2019 idadi ya wahamiaji wa kimataifa imeongezeka kutoka milioni 164 hadi milioni 169, sanjari na kuongeza idadi ya wafanyakazi wahamiaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina la Makadirio ya Kimataifa ya ILO kuhusu Wafanyakazi Wahamiaji: Matokeo na Mfumo” inaonyesha kwamba, mwaka 2019 wafanyakazi wahamiaji wa kimataifa walikuwa karibu asilimia tano wa wafanyakazi wote duniani na kuwafanya kuwa chachu muhimu ya uchumi wa dunia.

Ripoti iliongeza kuwa, miongoni mwa idadi hiyo wafanyakazi wahamiaji vijana wa umri wa kati ya miaka 15-24 wameongezeka pia kwa karibu asilimia mbili sawa na wafanyakazi milioni 3.2 tangu mwaka 2017 na kufikia mwaka 2019 idadi yao ilifikia milioni 16.8.

Licha ya idadi yao kuwa kubwa, ripoti imeweka wazi kwamba mara nyingi wafanyakazi hao wahamiaji wako katika ajira za muda, zisizo rasmi au zisizo na ulinzi hali ambayo inawaweka katika hatari kubwa ya usalama, kuachishwa kazi na kufanyakazi katika mazingira magumu.

ILO inasema na janga la virusi vya corona (COVID-19) limezidisha changamoto kwa wafanyakazi hao wahamiaji na hususani wanawake ambao idadi yao ni kubwa katika ajira zinazolipa ujira mdogo, kazi zisizo na ujuzi mkubwa na wana fursa ndogo sana ya ulinzi wa hifadhi ya jamii na hawana machaguo ya msaada wa huduma za msingi.

Kwa mujibu wa Manuela Tomei ambaye ni Mkurugenzi wa ILO Kitengo cha Hali ya Ajira na Ubora alisema,janga la COVID-19 limeanika hali mbaya ya wafanyakazi hao.

"Wafanyakazi wahamiaji mara nyingi ndio wa kwanza kuachishwa kazi, wanakabiliwa na changamoto kufikia huduma za matibabu na mara kwa mara wanaachwa katika mikakati ya kitaifa ya sera za kukabiliana na COVID-19,”alisema.

Pia kwa mujibu wa ripoti hiyo zaidi ya theluthi mbili ya wafanyakazi wahamiaji wamejazana katika nchi za kipato cha juu zikiongozwa na Ulaya na Asia ya Kati na kufuatiwa na Amerika, nchi za Kiarabu, Asia na Pasifiki na Afrika ikiwa na idadi ndogo zaidi.

Hata hivyo, asilimia kubwa ya wafanyakazi hao wahamiaji ni wanaume ambapo jumla yao ni milioni 99 huku wanawake ni milioni 70, huku wanawake wengi wakiajiriwa katika sekta za huduma zikiwemo za afya, kazi za majumbani, kulea wagonjwa na usindikaji wa vyakula huku wanaume wengi wakiajiriwa katika tasnia mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments