Serikali yatoa mwongozo wa udhibiti maambukizi ya Corona katika shule, vyuo na taasisi za elimu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Dodoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW) imeendelea kufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 nje na ndani ya nchi.

Hayo yamesemwa leo Julai 4, 2021 na Prof. Abel N. Makubi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wazara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati akizungumza jijini Dodoma.
Amesema, katika siku za hivi karibuni idadi ya wagonjwa imekuwa iongezeka kuashiria uwepo wa maambukizi kwenye jamii.

Hivyo, wizara ya afya imedhamiria kuhamasisha jamii kuongeza kasi ya kuzingatia utekelezaji wa afua za kudhibiti na kuzua maambukizi katika maeneo yote ya kutolea huduma yakiwemo maeneo ya shule. 

Amesema, kwa kuwa huu ni msimu wa kufungua shule na tupo kwenye tishio ni vema afua mbalimbali zikafuatwa.

"Kutokana na mahitaji mbalimbali kwa wakati wa sasa, Wizara imepitia upya Mwongozo wa udhibiti wa maambukizi ya COVID-19 katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini ulitolewa mwaka 2020 na ambao unaendelea kutumika hadi leo na kufanya maboresho machache.

"Mwongozo huu unalenga kuweka mazingira wezeshi katika maeneo ya Taasisi za elimu ikiwa ni pamoja na; vyuo, shule za sekondari, shule za msingi, shule za awali na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (day care centres) kabla ya wanafunzi kurejea shuleni na vyuoni kuendelea na masomo katika kipindi hiki ambapo bado kuna mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi aina ya Corona.

"Katika kufanikisha uwepo wa mazingira hayo, Mwongozo umezingatia maeneo makuu manne ambayo ni maandalizi ya mazingira na taasisi za elimu kabla ya kufunguliwa, cchunguzi wa Afya, ssafiri wa kwenda na kurudi shule na vyuo na mazingira ya kujifunzia kama inavyoonekana hapo chini:-

Maandalizi ya Mazingira ya Taasisi za elimu kabla ya kufunguliwa

Amesema, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara zote zinazosimamia vyuo na taasisi za mafunzo wanashauriwa kuhakikisha mazingira salama ya shule, vyuo na Taasisi za elimu kabla wanafunzi kurejea ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Katika kuandaa mazingira, mambo yafuatayo yanatakiwa kuzingatiwa;

Kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono kwa ajili ya usafi binafsi katika kila chumba cha darasa, ofisi, kila geti/lango kuu, kila bweni, maktaba, bwalo la chakula, vyoo na maeneo mengine muhimu.

Pia amesema, walimu na wakufunzi wapewe elimu juu ya mambo ya kuzingatia katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 katika maeneo ya kazi kabla ya kufungua shule, vyuo na taasisi.

Shule, vyuo na taasisi zenye vituo vya kutolea huduma za afya, watumishi wote wanaohusika wapewe elimu juu ya kuwahudumiwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote watakaoshukiwa kuwa na COVID-19 ikiwemo kuondoa unyanyapaa. Aidha, vituo vyote vinatakiwa viwe na dawa na vifaa kwa ajili ya dharura.

Wataalamu wa Afya wa Halmashauri wafanye ukaguzi katika shule, vyuo na taasisi za elimu ili kuhakikisha taadhari zote za kujikinga ma maambukizi ya COVID-19 zimezingatiwa kabla ya kufunguliwa na kutoa taarifa kwenye mamlaka husika.

Walimu wa Afya na Malezi (Guidance and Counseling Teachers) wapatiwe elimu ya utoaji wa Msaada wa kisaikolojia kwa ajili ya kusaidia wanafunzi, walimu pamoja na wafanyakazi katika eneo husika. Aidha, wanashauriwa kuwasiliana na wataalam wa afya walio karibu.

Uongozi wa shule, vyuo na taasisi za bweni uhakikishe kunakuwepo na nafasi ya kutosha (Mita moja) kati ya kitanda kimoja hadi kingine na kudhibiti uchangiaji vifaa kwa wanafunzi kama vile taulo, mashuka, vyombo vya kuogea na vifaa vya usafi wa mwili.

Uongozi wa shule, vyuo na taasisi uweke utaratibu mzuri wa upatikanaji wa barakoa katika maeneo yao kwa gharama nafuu. Aidha, kuhamasisha wazazi/walezi kuwapatia watoto wao barakoa na kuhakikisha walimu na wafanyakazi wote wanavaa barakoa muda wote wa kazi. Watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wenye magonjwa ya moyo, selimundu (sickle cell) mfumo wa hewa kama vile pumu na matatizo mengine ya kiafya hawaruhusiwi kuvaa barakoa.

Uongozi wa vyuo na shule utatakiwa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuhifadhia taka zitokanazo na barakoa zilizotumika na kuziteketeza kama taka nyingine hatarishi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Uchunguzi wa Afya;

Wanafunzi watakaohisiwa kuwa na dalili za kuumwa wafanyiwe vipimo kabla ya kurudi shule/chuo.

Amesema, wanafunzi watakaobainika kuwa na maambukizi wabaki nyumbani hadi hapo hali zao za afya zitakapoimarika.

Kwa wanafunzi ambao watabainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Korona wakiwa Shuleni/chuoni, Uongozi wa Shule au chuo utoe taarifa kwenye kituo cha huduma kilicho karibu na kumpeleka kwenye kituo husika kwa uchunguzi na matibabu

Usafiri wa kwenda na kurudi shule na chuo:

Amesema, wamiliki wa magari wahakikishe kuwa abiria na wahudumu wote wanavaa barakoa na kutumia kitakasa mikono kabla ya kupanda na wakati wa kushuka

Pamoja na kuvaa barakoa, wamiliki wa mabasi ya shule (School bus) waweke vitakasa mikono kwenye mabasi kwa ajili ya wanafunzi wakati wa kupanda na kushuka

Mazingira ya kujifunzia;

Uongozi wa shule na chuo unapaswa kuzingatia kuwa watumishi wote na wanafunzi wanakaa kwa umbali usiopungua mita moja kati ya mtu mmoja na mwingine wawapo sehemu yoyote wakati wa mafunzo

Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wengi, Uongozi uweke utaratibu mzuri wa wanafunzi kuingia madarasani kwa awamu (shifting).

Walezi wa mabweni (patron na matron) wapewe mafunzo na namna ya kubain ishara na mabadiliko ya mwanafunzi, pia wafanye ukaguzi mara kwa mara wa mabweni na afya za wafunzi.

Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu, walimu watatakiwa kuwa na barakoa maalum zitakazoruhusu mwanafunzi asiyesikia kuwasiliana na mwalimu.

Wanafunzi wenye ulemavu wanaohitaji usaidizi, wasaidizi na msaidiwa wavae barakoa na kutakasa mikono.

Walimu/wakufunzi na wafanyakazi wengine wote katika taasisi hizo wavae barakoa wakati wote wawapo shule.

Wanafunzi wa vyuo, Sekondari na shule za msingi wavae barakoa kipindi chote wanapokuwa darasani na wanapokuwa katika vikundi vya majadiliano ambapo inashauriwa kuzingatia kukaa umbali wa mita moja au zaidi na inapobidi wakati wa majadiliano wasizidi wanne.

Ziara za mafunzo zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na maambukizi
Wataalam wa afya ya jamii wahakikishe wanafundisha walimu na wafanyakazi wengine wa taasisi za elimu matumizi sahihi ya barakoa.

 Matumizi ya TEHAMA yanaweza kutumika katika kufundisha pale inapobidi kama itakavyoelekezwa na taasisi husika ili kupunguza uwezekano wa maambukizi.

Amesema, mwongozo huu utaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia hali ya mwenendo wa ugonjwa wa COVID-19 itakavyokuwa inaendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news