Wapendanao wafariki kwa kuweka jiko la mkaa chumbani kupunguza makali ya baridi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wapenzi wamefariki dunia mkoani Njombe.

Ni baada ya kuweka jiko la mkaa katika chumba walichokuwa wanalala ili kupunguza ukali wa baridi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Hamis Issa amesema watu hao wamefahamika kwa majina ya Benitho Mbata ambaye ni mkazi wa National Housing mjini Njombe na Jazira Said mkazi wa Namtumbo.

Amesema, wawili hao wamefariki dunia kutokana na gesi hatari ya mkaa na kuwataka wananchi kutafuta njia za kukabiliana na baridi ikiwemo kuvaa mavazi mazito badala ya kukoleza mkaa na kisha kuweka jiko vyumbani.

Mwenye nyumba, Samson Mwalongo na baadhi ya majirani wanasema kijana huyo hakuonekana kwa zaidi ya siku tatu hadi anatambulika kupoteza maisha na kudai kwamba hata mwanamke aliyepoteza maisha anadaiwa kuwa alikuwa safari kwenda Songea mkoani Ruvuma.

Mkoa wa Njombe kuanzia mwezi Juni hadi Septemba huwa ni kipindi cha baridi kali hivyo matumizi ya mkaa huongezeka zaidi katika familia mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments