WAVIU hatarini kuugua Corona-Ripoti

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi inaonyesha kuwa, watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wako katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).

Pia wanatajwa kuwa, wapo katika hatari zaidi ya kufariki dunia, lakini bado wananyimwa haki ya kupata chanjo dhidi ya COVID-19.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) mjini Geneva, Uswisi ambayo inajikita katika Kukabiliana na Ukosefu wa Usawa mwaka 2021 inaonyesha kuwa, ukosefu wa usawa unawafanya watu hao wanaoishi na VVU washindwe kupata chanjo dhidi ya COVID-19 na VVU.

Tafiti zilizofanyika Uingereza na Afrika Kusini zimeonyesha kuwa, hatari ya mtu anayeishi na VVU kufariki dunia kwa COVID-19 ni maradufu zaidi ya mtu asiye na VVU.

Aidha, katika nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako kuna asilimia 67 ya watu wote wanaoishi na VVU duniani kote, ni chini ya asilimia tatu ya watu hao ndio wamepata angalau dozi ya kwanza ya COVID-19 hadi Julai, 2021.

Pia imebainika kuwa, huduma za kinga dhidi ya VVU pamoja na matibabu zinaengua makundi muhimu na watoto na vijana balehe.

Ripoti hiyo inasema chanjo dhidi ya COVID-19 zinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, changamoto ni kwamba, chanjo zinahodhiwa na nchi tajiri na mashirika katika uzalishaji na usambazaji kwa lengo la kujipatia faida.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, kuna madhara makubwa katika mfumo wa afya kwenye nchi zinazoendelea kwani mifumo hiyo imezidiwa uwezo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima akizungumzia hali hiyo ya utata na sintofahamu kuhusu pengo la utoaji chanjo kati ya nchi tajiri na zile maskini amesema, “nchi tajiri barani Ulaya zinajiandaa kufurahia majira ya kiangazi kwa kuwa wananchi wao wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 wakati nchi maskini zipo katika janga.

"Dunia imeshindwa kupata somo kutokana na VVU wakati mamilioni ya watu waliponyimwa dawa muhimu za kuokoa maisha yao, walikufa kwa sababu ya ukosefu wa usawa. Hii haikubaliki,”amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news