Yanga SC yawatonesha Simba SC kidonda cha Januari 13

NA GODFREY NNKO

Zawadi Mauya ndani ya dakika ya 11 kwa shuti la umbali wa mita 21 kupitia pasi ya kiufundi ya kiungo mwenzake, Feisal Salum (Fei Toto) amewamaliza Wekundu wa Msimbazi, Simba SC na kuwapa Yanga SC alama tatu muhimu.
Ni kupitia mtanange wa aina yake ambao umepigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashuri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam leo Julai 3,2021.

Ni kwa ushindi huo, Yanga SC wamezima kelele za watani wao wa jadi, Simba SC baada ya kuwachapa bao hilo katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha alama 70 katika mchezo wa 31 na inabaki nafasi ya pili ikizidiwa alama tatu Simba SC ambao pia wana mechi mbili mkononi kwa sasa.

Leo Simba SC ilihitaji sare tu kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo na sasa watalazimika kusubiri hadi mechi ijayo.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ulitawaliwa na tambwe nyingi.

Wachezaji wanne wa Yanga walionyeshwa kadi za njano akiwemo kipa Faruk Shikalo, beki Adeyum Ahmed na viungo Mkongo Mukoko Tonombe na Feisal Salum.

Aidha,kwa Simba SC ni mabeki Mohammed Hussein (Tshabalala) na Mkenya Joash Onyango.

Leo ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baada ya ule wa Novemba 7, mwaka jana kumalizika kwa sare ya 1-1 hapo hapo Benjamin Mkapa, Yanga SC wakitangulia kwa bao la penalti la mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kipindi cha kwanza, kabla ya beki Mkenya Joash Onyango kuisawazishia Simba mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kipigo cha leo kinakumbushia machungu ya kichapo cha Machi 8, mwaka jana 1-0 pia hapo hapo Benjamin Mkapa bao pekee la Mghana ambaye sasa amehamia Simba, Bernard Morrison dakika ya 44, mchezo ambao ulihudhuriwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Aidha, kwa mwaka huu, Yanga SC imeipa kipigo cha pili Simba pamoja na ushindi wa Januari 13 wa penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Pia watani hao wanatarajia kukutana Julai 23, mwaka huu katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news