ACT Wazalendo waonyesha njia mapambano ya Corona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe licha ya kuipongeza Serikali kwa hatua ya kuruhusu chanjo ya corona kuingizwa nchini, lakini amesema kunatakiwa kuwapo na mkakati maalumu wa kuhamasisha wananchi dhidi ya corona ambao utaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii tofauti na ilivyo sasa.
"Niweke bayana kuwa, ni lazima kuwepo na mkakati maalum wa uhamasishaji dhidi ya Corona, mkakati ambao utaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii na sio watu wale wale ambao walituambia kuwa Tanzania imeshinda Corona, ama watu wale wale ambao walituaminisha kunywa tangawizi na malimao ni kutibu Corona;

Zitto ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya chama hicho mjini Unguja katika Jiji la Zanzibar.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kujadili hali ya kisiasa nchini huku akisema, hatua hiyo itasaidia badala ya kuendelea kuwatumia watu wale waliowaaminisha wananchi kuwa hakuna corona kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo.

Pia alitumia nafasi hiyo, kupongeza maamuzi sahihi ya kuruhusu chanjo iingizwe nchini ili kuwalinda wananchi wake na mfumo wa afya ambao bila kinga wengi hawataweza kujilinda.

"Nipongeze sana, lakini hatuwezi kuwa na utekelezaji bora wa sera mpya za kupambana na corona iwapo tutaendelea kuwa na sura zilezile zilizotuhaminisha kutumia njia zisizoshauriwa kisayansi. Nimatumaini yangu kuwa waziri wa sasa wa afya (Dkt.Gwajima na na naibu wake (Dkt.Mollel) na waziri wa sasa wa Katiba wa Sheria ambaye alikuwa wa Waziri wa Mambo ya Nje (Prof.Kabudi) wanapaswa kuwajibika au kuwajibishwa,”amesema Zitto.

Ameshauri pande zote mbili za serikali hatua mathubuti zichukuliwe kuongeza elimu kwa wananchi akisema mwaka mzima walikuwa wakiambiwa hakuna corona hivyo kuwambia sasa kwamba kuna corona sio jambo rashisi hivyo jitihada zifanyike kutoa elimu sahihi.

Zitto amesema, madhara ya corona nchini ni makubwa maana watu wanaendela kupoteza maisha na kwamba taarifa za Wakala Ufilisi na Udhamini wa Vifo (RITA) ya mwaka 2020 inaonyesha maombi ya kusajili vifo kupitia mfumo wa ehuduma yameongeza kufikia vifo 112,483 mwaka 2020 ikilinganishwa na vifo 35,000 mwaka 2019 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

Kiongozi huyo amesema, upo umuhimu wa wananchi kuendelea kuchukua tahahadhari zote zinazotolewa na watalaamu na licha ya kwamba chanjo kuwa hiari, lakini ipo haja wananchi kuchanjwa ili kunusuru wanaopoteza maisha.

Zitto amesema, corona haijaharibu maisha pekee bali pia imeharibu uchumi akisema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia zilizotolewa mwezi uliopita kasi ya ukuaji wa pato la taifa la Tanzania imeporoka kutoka asilimia saba mwaka 2019 hadi asilimia mbili mwaka 2020 huku Zanzibar ikitoka asilimia nane mwaka 2019 hadi asilimia 1.3 mwaka 2020.

Amesema, Corona imeathiri biashara na ajira ambapo asilimia 35 ya kampuni zimefungwa kati ya Januari 2020 na Janauri 2021 huku asilimia 17 ya wafanyakzi katika sekta ya utalii wamepoteza kazi zao kutokana na biashara kuwa ngumu kufungwa.

Wakati huo huo, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekanusha madai kuwa, amelishwa sumu kutokana na msimamo wake kuhusu chanjo ya virusi vya Corona.

Askofu huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyasema hayo wakati wa ibada kanisani kwake huku akisisitiza kuwa,hajalishwa sumu na hakuna wa kumfanyia hivyo.

“Wanataka kusingizia watu, labda kusingizia kwamba Serikali imeninywesha sumu. Niwahakikishie kwamba hakuna Serikali imemnywesha sumu Gwajima kwa kuwa serikali ndiyo inasema chanjo ni hiari. Hakuna wa kuninywesha sumu na hatotokea, labda nitoe changamoto kwa wanaojiita watalaam waje walete andiko linaloonyesha kemikali zilizopo kwenye chanjo,"amebainisha Askofu Gwajima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news