BENKI YA TCB YATOA MSAADA WA MADAWATI 50, DC NASSARI AHIMIZA WANANCHI UCHANGIAJI MAENDELEO

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

Tanzania Commercial Bank (TCB) imetoa msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi Milioni 6.5 kwa shule ya Msingi Maliwanda 'A' iliyopo kata ya Hunyari Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara.

Msaada huo unatokana na utaratibu wa kurudisha faida kwa wananchi ambao hufanywa kila mwaka ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Meneja wa Benki ya TCB tawi la Musoma, Hagai Gilbert akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 50 kwa Shule ya Msingi Maliwanda' A' kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda,Joshua Nassari na kulia kwake ni Afisa Elimu Msingi, Reginal Richard.(Picha na Diramakini Blog).

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Agosti 12, 2021 Meneja wa Benki ya (TCB) Tawi la Musoma, Hagai Gilbert amesema wameamua kutoa msaada huo katika shule hiyo kutokana na ombi lililowasilishwa kwao na uongozi wa shule hiyo ukitaka kusaidiwa madawati kutokana na uhaba mkubwa uliopo shuleni hapo na hivyo kupelekea baadhi ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini ya sakafu.

Hagai ameongeza kuwa, kutokana na hali hiyo TCB ndipo walipotoa madawati hayo ambapo yatasaidia kwa sehemu kupunguza changamoto ya wanafunzi kukaa chini, huku akisema utaratibu wa kusaidia jamii huduma mbalimbali utakuwa endelevu sehemu mbalimbali kulingana na uhitaji wa eneo husika kama ambavyo wamekuwa wakifanya kila mwaka.

"Shule hii wanafunzi wanakaa chini, ili mwanafunzi afanye vizuri zaidi katika masomo yake lazima awe na mazingira bora na rafiki ya kusomea, TCB kwa kutambua umuhimu wa elimu tumeona tutoe madawati haya kuunga mkono juhudi za serikali za kubooresha mazingira ya usomaji yawe mazuri. Niombe pia wadau wengine wajitokeze kusaidia popote walipo," amesema Hagai.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Bunda, Reginald Richard akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bunda, ameishukuru TCB kwa msaada huo ambapo amesema utachochea ufanisi wa taaluma shuleni hapo. Huku pia akisisitiza wazazi kujenga utaratibu wa kushiriki katika uboreshaji wa mazingira bora ya wanafunzi kusomea ikiwemo kuchangia madawati na ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa hiari.

"Mwanafunzi anapokaa chini wakati mwalimu anafundisha darasani ni vigumu kuelewa kinachofundishwa, kwa hiyo picha ni kwamba ili asome vizuri ni lazima akae kwenye dawati aandike vizuri tofauti na chini ambapo pia vumbi na vikwazo vingine vinamfanya asisome vizuri. Niwaombe wadau wote tushiriki kwa pamoja kutatua tatizo la madawati ambalo ni kubwa shuleni hapa," amesema Richard.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari akizungumza mara baada ya kupokea madawati 50 kutoka Benki ya TCB kwa ajili ya Shule ya Msingi Maliwanda 'A' iliyopo Bunda. Kulia kwake ni Meneja wa TCB tawi la Musoma, Hagai Gilbert.(Picha na Diramakini Blog).

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Nassari ambaye alikuwa mgeni rasimi katika zoezi hilo, mbali na kupongeza TCB kwa msaada huo. Amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa kero mbalimbali katika maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo serikali pekee.

Nassari amesema, kwa kipindi ambacho amekuwa mkuu wa wilaya hiyo, kila anapokwenda amekuwa akikuta baadhi ya shule zina upungufu wa matundu ya vyoo na madawati na kupelekea wanafunzi kukaa chini, lakini wananchi wa eneo husika wana rasilimali nyingi ikiwemo mifugo. Na hivyo akawataka waachane na zana potofu kuwa serikali pekee itatatua kero hizo badala yake amewasisitiza washiriki kuchangia maendeleo katika maeneo yao.

"Bunda wananchi hawashiriki katika shughuli za maendeleo kabisa, ni aibu kubwa shule unakuta ina upungufu wa matundu ya vyoo na madawati wakati watu wana mifugo kwa wingi. Wilaya ya Bunda ina watu wengi mashuhuri serikalini, jeshini, wafanyabiashara na katika siasa nikuombe Afisa Elimu Wilaya uandae orodha yao yote unipatie kusudi niwatafute washiriki kuchangia maendeleo ya Bunda. Sipo tayari kuwa mkuu wa Wilaya katika eneo lisilo na maendeo lazima tuyalete kwa pamoja bila kuiachia jukumu hili serikali pekee," amesema Nassari.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari katikati akikata utepe kama ishara ya kupokea msaada wa madawati 50 kutoka Benki ya TCB mwenye suti nyeusi ni Meneja wa TCB Tawi la Musoma, Hagai Gilbert na viongozi mbalimbali.(Picha na Diramakini Blog).

Dorcas Lameck ni Mwanafunzi wa darasa la tatu shuleni hapo, ambapo amesema kutokana na kusomea chini wakati mwingine usomaji unakuwa mgumu hasa wakati wa kuandika na hivyo ameishukuru TCB kwa kuwakumbuka na ameomba taasisi mbalimbali kuiga mfano huo katika kusaidia sekta ya elimu kuandaa wasomi bora watakaolitumikia taifa kwa siku za usoni kuliletea maendeleo.

Juma Mathias ni Mkazi wa Maliwanda ambapo amesema kitendo kilichofanywa na TCB kina mchango mkubwa katika kuinua ufaulu na sekta ya elimu kwa ujumla. Na hivyo ameomba wananchi kufungua akaunti katika Benki hiyo ili kuiunga mkono pamoja na kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za mikopo mbalimbali.
Wanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya Msingi Maliwanda ' A' wakiwa wamekaa wakisoma kutokana na ukosefu wa madawati. Benki ya TCB imetoa msaada wa madawati 50 kusaidia kutatua changamoto hiyo huku madawati 183 yakihitajika.(Picha na Diramakini Blog)

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maliwanda 'A' Fredrick Vincent akisoma taarifa ya shule hiyo, amesema ina jumla ya wanafunzi 753. Huku akisema kwa kiwango kikubwa inakabiliwa na upungufu wa madawati 183, matundu 10 ya vyoo vya wanafunzi, nyumba 15 za walimu, uchakavu wa madarasa, pamoja na ukosefu wa chumba cha TEHAMA akaomba serikali na wadau kushiriki katika utatuzi wa changamoto hizo.

Post a Comment

0 Comments