DC JOSHUA NASSARI ASISITIZA UAMINIFU KWA WAFANYABIASHARA BUNDA ULIPAJI KODI

Na Fresha kinasa, Diramakini Blog

Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Joshua Nassari amewataka wafanyabiashara wilayani humo kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu.

Hatua ambayo itaiwezesha Serikali kutekeleza shughuli za utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na maendeleo kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, Joshua Nassari. (Picha na Diramakini Blog)

Nassari ameyasema hayo Agosti 11, 2021 wakati akifungua mafunzo katika mkutano wa wafanyabiashara ulioandaliwa na TRA Mkoa wa Mara kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu mabadiliko ya sheria mpya za kodi kwa mwaka 2021/ 2022 pamoja na matumizi ya mashine za kielektroniki. Ambapo yamefanyika katika ukumbi wa Land Master Hotel wilayani humo.

Nassari amesema kuwa, ili Serikali ifikie malengo ya utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi lazima iwe na fedha za kutosha ambazo zitasaidia utoaji wa huduma hizo. Hivyo amewasisitiza wafanyabiashara kutojihusisha na tabia ya ukwepaji wa kodi pindi wanapotoa huduma kwa wateja sambamba na uzingatiaji utoaji wa risiti kwa uaminifu.

"Zingatieni ulipaji wa kodi mnapotoa huduma ikiwemo kodi za mabango na ushuru wa huduma, kodi hizi ndizo zinasaidia ujenzi wa barabara, uboreshaji wa barabara, utoaji elimu bure, ununuzi wa dawa na huduma zingine. Serikali haiwezi kuyatekeleza haya bila watu kulipa kodi kwa uaminifu," amesema Nassari.
Aidha, Nassari amewataka wafanyakazi wa TRA kutenda haki katika kazi yao sambamba na kufanya kazi kwa uadilifu na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kudhoofisha makusanyo ya kodi na kupelekea serikali kutofanya majukumu yake kwa ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

"Kama kuna changamoto yoyote ambayo wafanyabiashara mnadhani kwamba itawakwamisha kufikia malengo yenu. Ofisi yangu ipo wazi muda wote kuwapa ushirikiano wa namna bora ya kupiga hatua kwenda mbele zaidi ili mfanye biashara kwa ufanisi,lakini pia mlipe kodi kwa maendeleo ya nchi,"amesema Mkuu huyo.
Afisa Elimu Huduma kwa mlipa kodi Mkoa wa Mara,Zake Wilbard aliyesimama akitoa semina ya mabadiliko ya sheria ya kodi kwa mwaka 2021/2022 kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Bunda. Ambapo mafunzo hayo yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Joshua Nassari.

Kwa upande wake Afisa Elimu na Huduma kwa mlipa kodi kutoka TRA Mkoa wa Mara,Zake Wilbard Rwiza amesema miongoni mwa malengo ya mabadiliko ya sheria ya kodi kwa mwaka 2021 / 2021 ni kufufua kasi ya ukuaji wa uchumi kutokana na madhara ya ugonjwa wa Corona sambamba na kuimarisha mfumo wa kodi unaotabirika kwa mazingira ya uwekezaji.

Pia amesema ni kuweka, kutoza au kubadilisha baadhi ya kodi, tozo na ada pamoja na kurekebisha sheria zingine zinazohusu ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya umma.

Ameongeza kuwa, bajeti ya serikali kwa mwaka 2021/2022 ni kukusanya sh. trilioni 36.33 ambapo TRA inatakiwa kukusanya sh.22.18 trilioni. Huku lengo la makusanyo ya mwaka huu akisema ni zaidi kwa shilingi trilioni 1.85 kulinganisha na lengo la mwaka jana.

Mathayo Machiru ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Mji wa Bunda, amesema kulipa kodi kuna faida kubwa kwani Wafanyabiashara na wananchi watakuwa na uhuru wa kuhoji hata pindi maendeleo yanapochelewa kufanywa na serikali.

Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Robert Maboto ameishukuru TRA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa Wafanyabishara, ambapo amesema kwa sasa wafanyabiashara waondoa zana ya kufanya biashara bila kulipa kodi bali suaka la kodi walipe kipaumbele kwani linatija kwa maendeleo ya nchi na linawapa uhuru wafanyabiashara wa kufanya kazi zao.

Juma Mathias na Prisca Joashi wafanyabiashara wa Bunda wamepongeza mafunzo hayo ambapo wamesema yamewaongezea ujuzi, upeo na maarifa mengi katika utekelezaji wa majukumu yao. Ambapo changamoto zao pia zimetatuliwa kupitia majibu kutoka kwa Wataalamu wa TRA huku wakiahidi kuendeleza mahusiano mema na Mamlaka hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news