Fundi rangi mbaroni kwa tuhuma za ugaidi mkoani Songwe

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia na kumhoji mwanaume mmoja jina limehifadhiwa ambaye ni mkazi wa Lushoto Mkoa wa Tanga kwa tuhuma za ugaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi ameyasema hayo Agosti 3, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amedai kuwa,mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 2, mwaka huu majira ya saa 10 jioni katika moja ya mgahawa katika mji wa Vwawa huko wilayani Mbozi mkoani hapa.

Kamanda Magomi amesema, mtuhumiwa huyo alikamtawa na jeshi hilo kwa kushilikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama baada ya kupokea taarifa za siri kutoka kwa raia wema akiwa katika harakati za kusafiri kuelekea nchini Zambia.

Amesema, mtuhumiwa huyo baada ya kufanyiwa upekuzi wa awali alikutwa na vitu mbalimbali, ikiwemo hati ya kusafiria ya Tanzania ambayo inaonyesha kuwa kwa nyakati tofauti mtuhumiwa huyo amesafiri katika nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Tanzania.

“Hatuwezi kuthibitisha kuwa ni gaidi kwa kuwa bado tunaendelea kumfanyia mahojiano, japo kuna viashiria ambavyo vinatupa mashaka hususani kupitia hati yake ya kusafiri ambayo imeonyesha kufanya safari nyingi na za mara kwa mara katika nchi hizo nilizozitaja, pamoja na orodha ya namba za simu,”amedai Kamanda huyo.

Ametaja vitu vingine alivyokamatwa navyo mtuhumiwa huyo kuwa ni simu za mkononi nane ambazo zote hazikuwa na laini.

Sambamba na mkoba mdogo wenye nguo chache ambazo nyingi zikiwa ni chakavu.

Pia Kamanda Magomi alidai, katika upekuzi huo, mtuhumiwa alikutwa na orodha ndefu ya namba za simu za watu tofauti tofauti kutoka mataifa aliyosafiri kwa mujibu wa hati yake ya kusafiria, pamoja na mataifa mengine ya nchi za Mashariki ya Mbali.

“Katika mahojiano ya awali mtuhumiwa huyo ambaye amejitambulisha kuwa yeye ni fundi rangi tumemkuta na fedha taslimu shilingi 25,000 tu na amesema kuwa amekuwa akienda katika nchi hizo kwa shughuli za upakaji rangi kwenye nyumba,”amedai Kamanda huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news