Jela maisha kwa kumbaka mtoto wa mwaka mmoja

NJOMBE, Mahakama ya Wilaya ya Njombe imemuhukumu kifungo cha maisha, Steward Mkongwa (33) kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba.
Katika shauri namba 42 la mwaka 2021 mshtakiwa anadaiwa kufanya kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili lakini pia kifungu 131 kifungu kidogo (1)(3) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Inadaiwa kuwa mnamo tarehe 26 mwezi Julai mwaka 2020 katika Mtaa wa Mwembetogwa wilayani Njombe mshtakiwa alimbaka mtoto mwenye umri huo.

Shauri hilo lililosimamiwa na wakili wa Serikali, Matiko Nyangero lilikuwa na mashahidi wanne upande wa mashtaka na shahidi mmoja upande wa utetezi ambaye ni mshtakiwa katika kesi iliyoendeshwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, Isaack Mlowe.

Hakimu Mlowe alisema mshtakiwa alikiri kufanya kitendo hicho cha kumuingilia mtoto huyo baada ya mama yake kwenda kuchota maji.

"Alifanya hivyo kwa sababu yeye alikuwa mpangaji pamoja na mama wa huyo pia alikuwa na mazoea na huyo mtoto," alisema Mlowe.

Kabla ya hukumu hiyo mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea alisema yeye ana familia inamtegemea kwani ana watoto wawili wa kuwazaa na watoto sita aliyeachiwa na marehemu kaka yake.

Alisema mke wake aliachana naye kutokana na mitafaruku mbalimbali hivyo mpaka sasa hafahamu watoto hao wanakula ama la.

"Mimi mwenyewe miguu yangu yote miwili ni mibovu kutokana na kuwa nilipata ajali," alisema Steward.

Baada ya utetezi huo hakimu Mlowe alimuhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha maisha kutokana na kifungu cha sheria namba 131(3) kinachosema mtu yeyote anapotiwa hatiani kwa kosa la ubakaji kwa mtu mwenye umri wa miaka chini ya kumi adhabu yake ni kifungo cha maisha. (Mwananchi)

Post a Comment

0 Comments