Mashirika 1,500 kushiriki Maonesho ya Wiki ya Azaki Oktoba 23-29 jijini Dodoma

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Haki Rasilimali, Racheal Chagonja amesema kuwa, mashirika zaidi ya 1500 yatashiriki katika Maonesho ya Wiki ya Azaki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 mpaka 29 mwezi Oktoba, mwaka huu jijini Dodoma.
Chagonja amebainisha hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Wiki ya Azaki kwa mwaka 2021.

Amesema, maonesho hayo tangu yameanza kufanyika nchini mwaka 2018, yamesaidia wananchi kupata uelewa mpana kuhusu kazi zinazofanywa na Azaki mbalimbali nchini.

“Toka tumeanza kufanya maonyesho haya tumepata mafanikio makubwa sana ikiwemo wananchi kutambua nini Azaki zinafanya nchini, lakini mwaka jana kutokana na changamoto ya ugonjwa wa UVIKO-19, hatukuweza kuyafanya lakini hali hiyo imetuwezesha kujipanga kwa ajili ya kutathimini mapungufu na kuja kivingine mwaka huu,”amesema Chagonja.

Amesema, Wiki ya Azaki mwaka huu itajumuisha pia maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika hayo ikiwemo uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

“Kutakuwa na siku mbili ya kuonyesha bidhaa zinazaozalishwa na asasi mbalimbali maonesho haya yatafanyika Oktoba 23 na 24 katika viwanja vya Jamhuri na baada ya hapo tutakuwa na midahalo ya ndani kuhusu mambo mbalimbali,”amesema.

Aidha, amesema lengo la wiki hiyo pia itakuwa pia ni kujenga ushirikiano baina ya serikali, wadau,mashirika binafsi pamoja na wanachi katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Tunashukuru hivi sasa wananchi wameweza kutambua umuhimu wa Asasi hizi za kiraia katika kuleta maendeleo kwenye jamii zetu hivyo wiki hii mwaka huu tutaitumia kuendeleza kile ambacho tumekuwa tukikifanya katika miaka iliyopita,”amesema Chagonja.

Kadhalika, alisema pia katika wiki hiyo mwaka huu pamoja na mambomengine pia kutakuwepo na huduma za msaada wa kisheria zitakazotolewa kwa wanachi wenye uhitaji na mashirika mbalimbali.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM International Tanzania, Nesia Mahenge amesema, katika wiki hiyo watahakikisha kuwa tahadhari zote za kujilinda na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO 19, zinachukuliwa ipasavyo.

“Niwahakikishie washiriki wote pamoja na wananchi kuwa tahadhari dhidi ya maambuzi ya virusi vya ugonjwa wa corona yatachuliwa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wetu wa afya,”alisisitiza Mahenge.

Kwa upande wake Shaki Shalaji ambaye ni mwakilishi Msajili wa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali NGO's kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, amesema, katika wizara wana sera ya 2011 ya kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi ili waweze kufanya kazi kwa weledi.

Amesema kuwa, mashirika haya yatazingatia utaratibu wote ulioanishwa na Wizara ya Afya huku wakilindwa kwani mashirika hayo yamekuwa yanafanya kazi kubwa na Serikali kutoa elimu, kuweka vitakasa mikono na kutoa elimu mbalimbali.

Awali akizungumza na vyombo vya habari Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga amesema, kwenye maonyesho kutakuwa na wigo mpana na lengo mojawapo ni kusherehekea yale waliyoyafanya kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwa maonyesho hayo mwaka 2018 huku kauli mbiu ikiwa ni "Mchango wa Asasi za Kiraia ni Kujenga Nchi".

Pia amesema lengo lingine ni kuondoa mtazamo uliojengeka kwenye akili za watu kwamba mchango wa Azaki sio mkubwa sana na kutambua umuhumu wake kwani tangu wamefanya maonyesho kumekuwa na mwitikio mkubwa sana kwa jamii.

"Licha ya hayo lengo la Maonesho ya Wiki ya Azaki ni kuboresha mahusiano yaweze kujengeka vizuri kati ya sekta mbalimbali na jamii kwa ujumla, hivyo niwasihi Watanzania kuja kwenye maonyesho hayo ambapo kutakuwa na burudani za tamaduni mbalimbali na kutambua mchango wa kila mtu,"amesema Kiwanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news