Mguu kwa Mguu ziara ya Mwenyekiti CCM Mara, RC ilivyofichua madudu

*Wananchi wampongeza, Tarime yaongoza, asisitiza hana kundi zaidi ya lile la Rais Samia Suluhu Hassan

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

ZIARA ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) na Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi imeibua madudu mbalimbali katika halmashauri za mkoa huo huku Tarime ikiongoza.

Hayo yamebainishwa baada ya kubainika kuwa, kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha katika miradi ya maendeleo hususani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mwenyekiti huyo amemshauri mkuu wa mkoa kuchukua hatua.
Pia amesisitiza kuwa, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao watajihusisha na vitendo vya rushwa watashughulikiwa bila kujali nafasi ya mtu mkoani humo.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (Ally Hapi) wachukulie hatua watu waliofanya ubadhirifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, watu wa manunuzi pamoja na wenye maduka,pale wamenunua tofali moja kwa sh.2,500. Hawa ni wezi wakubwa ,wakamatwe haraka hatuwezi kuvumilia vitendo kama hivi," ameeleza Mwenyekiti Kiboye.

Aidha,Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mara, Samwel Kiboye akiwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa Mara, Ally Hapi walikagua huduma mbalimbali zinazotolewa katika Hospitali ya Kwangwa ikiwemo huduma ya upandikizaji wa figo iliyoanza kutolewa katika hospitali hiyo iliyopo Manispaa ya Musoma

Kiboye alichukua nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele miradi ya maendeleo ikiwemo huduma za afya ambazo zimeendelewa kutengewa fedha nyingi ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Hatutakubali kuona watu wanacheza na kumdharau Rais wetu,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, sasa hivi kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) tumejipanga kweli kweli,hatukokubali watu wanaobeza shughuli za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan. Kila mmoja wetu ni shaidi, kazi zinafanyika tena kwa kasi kubwa, hivyo wabadhirifu na wabezaji hawana nafasi kabisa,"amesema Kiboye.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo amekielekeza chama hicho kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya mkoa huo hasa kumuunga mkono mkuu wa mkoa Mara, Ally Hapi kutokana na kuonyesha nia njema ya kuijenga Mara mpya.

Kiboye aliwapongeza wenyeviti wa chama hicho ngazi ya wilaya katika Mkoa Mara kwa kujitolea na kuhudhuria ziara ya Mkuu wa Mkoa Mara, Ally Hapi huku akishangazwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime kutohudhuria kabisa.

"Ninalaani vikali kitendo cha viongozi wa chama CCM wilaya Tarime kutohudhuria ziara ya Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Ally Hapi alipokuwa katika wilaya ya Tarime,nimekereka zaidi na mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daud Ngicho kutokuwepo kabisa,"alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mara, Samwel Kiboye alisema kuwa, kundi lake ni la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na hana kundi lolote lingine. "Nina kundi moja tu la Rais wetu Samia Suluhu Hassan na wewe uvunje makundi yote ubaki na kundi la Rais tu,"alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa, amejipanga kuijenga Mara mpya hivyo, ushirikiano utamuwezesha kufanikisha lengo hilo kwa muda mfupi.

"Nimejipanga kuijenga Mara mpya na nimezunguka ziara yangu katika huu mkoa mzima, nimegundua kuna changamoto nyingi sana. Nataka niwaambie ndugu zangu wananchi,nitawachukulia hatua watendaji wa Serikali ambao hawatatui kero za wananchi,"alisema RC Hapi.

Pia RC Hapi aliwaonya watendaji wa Serikali ambao hawasikilizi na kutatua kero zinazowakabili wananchi katika mkoa huo huku akisisitiza watumishi hao kutokaa ofisini badala yake wawatembelee wananchi huko walipo ili watatue kero zinazowakabili.


MUHIMU

UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news