Mkakati wa kuidhibiti Corona sokoni washika kasi mkoani Dodoma

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Uongozi wa Soko la Sabasaba jijini hapa umepiga marufuku mtu yeyote kuingia ndani ya soko hilo bila kuvaa barakoa,jambo ambalo litasaidia wananchi kujikinga na maambukizi ya virusi vya CORONA.
Mkakati huo umeandaliwa na uongozi wa soko la Sabasaba kwa kushirikiana na afisa afya wa kata ya Viwandani huku wakiwa wameweka maji tiririka,vitakasa mikono, wauzaji wa barakoa na mgambo kila mlango wa kuingilia sokoni humo.

Akizungumza na DIRAMAKINI BLOG Kaimu Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Adam Kombo amesema, kwa pamoja uongozi umeshaweka msimamo kuwa ni lazima kila mtoa huduma avae barakoa na anayepatiwa huduma pia avae barakoa.

"Tumeweka utaratibu wa kuhakikisha watu wote ambao wanaingia katika soko la Sabasaba wanakuwa wamevaa barakoa.

"Tumeweka maji tiririka kila mlango wa kuingilia,tumeweka vitakasa mikono na kila mlango kuna watu ambao wanauza barakoa na zaidi ya yote kuna mgambo kila mlango ambaye kazi yake kubwa ni kuwazuia watu wasiokuwa na barakoa wasiingie ndani ya soko.

"Hatuwezi kuwa wapole kwa jambo hili ni bora tuwe wakali watu watuchukie kuliko kuwa wapole na kutafuta sifa wakati wapo watu wanaangamia,"amesema Kombo.

Kwa upande wake Afisa Afya Kata ya Viwandani jijini Dodoma, Fausta Kibiti amesema kwa kutekeleza maagizo ya mkuu wa mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka ya kutaka watoa huduma na wanaopatiwa huduma kuvaa barakoa sasa wanalitekeleza kwa vitendo.

"Uongozi wa ofisi ya Afya Kata ya Viwandani kwa kushirikiana na uongozi wa soko la Sabasaba tunaendesha opareisheni ya kuwataka watu wote wavae barakoa.

"Tumekuwa na operesheni kwa wale ambao wanauza mitumba kwa kuwataka wavae barakoa na wanaokaidi wanatolewa na mgambo ndani ya soko.

"Tunatoa elimu juu ya umuhimu wa kuvaa barakoa na ikumbukwe kuwa katika magulio kuna msogamano mkubwa ambao ni hatari kwa afya ya watoa huduma na wapokea huduma.

"Hili zoezi ni endelevu na nilazima lifanyike mara kwa ara kwa faida ya wafanya biashara na wanaopata Mahitaji katika soko la sabasaba,"ameeleza Fausta.

Aidha DIRAMAKINI Blog imetembelea Soko Kuu la Ndugai jijini hapa pamoja na soko la Majengo kujionea hali halisi ambapo imeonyesha dhahiri kuwa tayari elimu ya kujingika na maambukizi ya Corona imewafikia wengi kutokana na vifaa vyote kuwepo Katika masoko hayo.

Amos Faustine ni Katibu wa Soko la Ndugai amesema kuwa,wao walianza utaratibu huo tangu mwaka jana ambapo kila mtu anayefika eneo la soko ni sharti anawe mikono japo kwa upande wa barakoa ilikuwa kazi kubwa kutoa elimu ila kwa sasa wameelewa.

Nae Mwenyekiti wa soko la Majengo jijini hapa, Mathayo Mollel amesema kuwa, hapo awali wafanyabiashara walikuwa wabishi kutovaa barakoa na wengine Kutoa sababu ambazo sio za msingi ndipo uongozi uliweka sheria kwa wasiovaa jambo ambalo lilisaidia wengi kutii amri na mpaka sasa hali ni nzuri wanajikinga.

Baadhi ya wafanyabiashara na wateja katika soko la Sabasaba na Majengo kwa nyakati tofauti wamesema kuwa, utaratibu wa kuvaa barakoa ni mzuri kwani ni kwa faida ya mtu mmoja mmoja na kuzuia maambukizi kwa mtu mwingine.

"Tunaona utaratibu huu wa kuvaa barakoa na kunawa mikono ni utaratibu ambao unafaa kuzingatiwa bila hata kulazimishwa kwani kwa sasa hali ya ugonjwa ni mbaya na ukizingatia hii mikusanyiko ni lazima kuvaa barakoa,"wamesema wafanyabiashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news