BILIONI 28/- KULIPA FIDIA MIKOA LINAPOPITA BOMBA LA MAFUTA

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) linatarajia kulipa fidia wananchi 9,122 jumla ya Shilingi Bilioni 28 katika mikoa nane inayopitiwa na Bomba la Mafuta ili kupisha mradi huo.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza katika kongamano la fursa za Bomba la mafuta Wilayani Chato liloandaliwa na TPDC. (Picha na Robert Kalokola).
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Martha Mkupasi akizungumza katika kongamano la fursa za Bomba la mafuta wilayani hapa.(Picha na Robert Kalokola).

Amesema hayo katika kongamano la viongozi wa serikali,wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wananchi ambalo limefanyika katika Kijiji cha Mkungo wilayani Chato kwa kuandaliwa na TPDC likiwa na lengo la kutambua fursa katika ujenzi wa bomba hilo la mafuta.

Amesema, mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitatu, ambapo wananchi watapata fursa mbalimbali za kiuchumi katika mikoa hiyo minane nchini ambayo mradi huo utapita, bomba lenye urefu kilomita 1,147 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Washiriki katika kongamano la fursa za Bomba la mafuta wilayani Chato. (Picha na Robert Kalokola).

Aidha, ameitaka TPDC kulipa fidia wananchi ili ujenzi wa bomba hilo la mafuta uanze mara moja mwezi ujao ili wananchi waanze kunufaika na fursa zilizopo.

Waziri amesema fursa hizo za uwekezaji zichukuliwe na wazawa wa maeneo husika linapopita bomba hilo na kwamba hatafumbia macho urasimu wa aina yoyote katika utoaji wa fursa hizo.

Aidha, Waziri Kalemani amewataka wananchi watakakaolipwa kwa ajili ya kupisha mradi kuondoka mara moja ili mradi uendelee na si kudai fidia mara mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dkt. James Mataragio akizungumza katika kongamano la fursa za Bomba la mafuta wilayani hapa.(Picha na Robert Kalokola).

Mkurugenzi mkuu wa TPDC, Dkt. James Mataragio amesema kuwa hadi Sasa shirika hilo limeishalipa fidia kwenye kambi saba.

Ameeleza kuwa, kwa sasa shughuli inayofanyika ni kazi ya kupata wakandarasi wakubwa ambao baada ya kusaini mikataba nao ndio watafungua fursa zaidi kwa kusaini mikataba midogo na wawekezaji wa ndani.

Dkt. Mataragio ameongeza kuwa, kuna fursa zitapatikana kwenye mafuta kwa sababu sasa hivi unafanya utafiti unafanyika katika mikoa ya Shinyanga,Singida,Simiyu, Manyara na Arusha ambapo wanakaribia kuanza uchorongaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news