MUHOJI AFUNGUA KIKAO KAZI KATI YA TUME NA WADAU KUJADILI MPANGO MKAKATI WA MWAKA 2021/22- 2025/26

Na Mwandishi Maalum-PSC

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Nyakimura Muhoji leo amefungua Kikao Kazi kinachofanyika mkoani Morogoro kati ya Tume na Wadau kujadili Mpango Mkakati mpya wa Tume wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 ulioandaliwa baada ya kuhuisha Mpango Mkakati uliokuwepo awali wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bwana Nyakimura Muhoji (wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki baada ya kufungua Kikao kazi leo kujadili Mpango Mkakati wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kipindi cha 2021/22-2025/26, kinachofanyika Mkoani Morogoro. (Picha na PSC).

Muhoji amesema kuwa majukumu yaliyo kasimiwa kwa Tume ya Utumishi wa Umma ndiyo yanaipa Tume uhalali wa kuwa na Mpango Mkakati huu ulioandaliwa. Amewakumbusha washiriki kuwa kazi kubwa ya Tume ni kuhakikisha kwamba katika Utumishi wa Umma panakuwepo na Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu.

“Majukumu haya yameainishwa katika Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 (Marejeo ya mwaka 2019). Baadhi ya Majukumu haya ni:- Kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma; Kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumishi na rufaa za mashauri yaliyotolewa uamuzi na Mamlaka za Nidhamu; Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia matokeo; na Kuhakikisha kuwa Taratibu za Uendeshaji za Utumishi wa makundi mbalimbali ya kiutumishi zinatayarishwa na kutumika ipasavyo,” alifafanua Bw. Muhoji.

Alisema kuwa, pamoja na mabadiliko ya Muundo wa Tume uliopitishwa na kuidhinishwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2018, bado Tume iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutumia Mpango Mkakati uliokuwepo. 

Hivyo, ushirikishaji wa wadau katika Kikao kazi hiki ni moja ya hatua muhimu katika uandaaji wa Mpango Mkakati, maana Wadau ni jicho lingine la Tume kwa kuwa sote tunafahamu kuwa hatuwezi kujitathmini wenyewe tukapata kitu bora bila kumshirikisha yule tunayemhudumia, tunafahamu pia kuwa upo mchango kutoka kwa wadau wetu katika kuuboresha Mpango Mkakati huu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. David Pwele alisema Tume imeandaa kikao kazi hiki kwa lengo la kujadili, kufanya tathmini na kujiridhisha kama Mpango Mkakati huu umegusa vya kutosha huduma inazozitoa kwa wadau wake kupitia majukumu ya Tume ambayo imepewa kwa mujibu wa Sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news