Mwenyekiti CCM Mara achanja chanjo ya UVIKO-19 asisitiza yupo imara, ampongeza Rais Samia kwa ujasiri

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) amekuwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama mkoani hapa kuchanja chanjo ya virusi vya Corona huku akiwataka Watanzania na wana Mara kuendelea kuchangamkia fursa hiyo kwa ajili ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Ametoa wito huo leo Agosti 6, 2021 mjini Tarime baada ya kuchanja chanjo ya Corona huku akiwapongeza wataalam wa afya pamoja na Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha inatafuta kila njia kuwakinga wananchi wake.

"Ninashukuru Mungu kwa sababu hii chanjo imekuja na itasaidia watu, lakini tuendelee kujikinga hata kama tumechanjwa, kwa sababu chanjo si kwamba inatibu bali ina kinga,"amesema Kiboye.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mara ametaja miongoni mwa tahadhari nyingine ambazo kila mwananchi anapaswa kuzichukua kuwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kutakasa mikono, kunawa mikono na maji tiririka kwa kutumia sabuni, kuepuka misongamano na miongozo mingine kadri inavyotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya nchini.

"Kwa sababu hata zamani walituchanja pepo punda, walituchanja surua, lakini naomba watu wasipinge chanjo, kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hawezi kutuletea kitu cha kuua watu, lazima ajue kwamba Watanzania ni watu wake.

"Na wale watu ambao wanahamasisha watu kwamba chanjo ni mbaya, naomba waache mara moja, wao kama hawataki kuchanjwa waache, waache watu wachanjwe kwa sababu kuchanjwa ni hiyari ya mtu, sasa wasizuie watu, ninaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuchanjwa.

"Mimi kama mwenyekjiti wa mkoa leo nimepata chanjo yangu hapa, na nimechanja Tarime na nimeamua kuchanja hapa ili wana Tarime waone, kwa sababu ndiyo ninaishi na ndiyo nyumbani, watambue kwamba hii chanjo ni ya watu wote.

"Na ninashukuru madaktari na manesi ambao wanaendelea kuchanja, wapo 'serious' na wanachanja. Tunaomba wale wazee kuanzia miaka siti, miaka hamsini na miaka sabini na kuendelea wajitokeze kwa wingi na hata vijana wajitokeze kuchanjwa.

"Kwa sababu hii chanjo ni kwa watu wote, kwa hiyo tuendelee kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu chanjo, hata sasa hivi ninakimbia kuelekea kijijini kule Shirati kuwachukua wazee wangu ili waje wachanjwe, kwa sababu mama na baba wameshakuwa wazee ili wachanjwe kwa sababu hii chanjo ni kinga ambayo inatusaidia.

"Kama tulivyochanjwa surua, homa ya manjano, homa ya ini. Chanjo siyo kwamba ina madhara,hapana...wanaotaka kugeuza hii chanjo kama kitu chenye madhara waache,lakini tunapochanjwa tuendelee kumuomba Mungu kwa jina la Yesu itatoka hii Corona.

"Tumuweke Mungu mbele ili hii Corona itoke kwa jina la Yesu Kristo na Mungu wa Mbinguni aitawanyishe hii Corona. Na Mungu aendelee kuisambaratisha hii Corona, umeona Tarime watu wamejitokeza kwa wingi kuchanjwa, lakini pia katika mkoa wa Mara watu wameendelea kujitokeza wengi sana, hivyo tusimpinge Rais, tuendelee kumuunga mkono, na Mungu wa mbinguni awabariki sana,"amefafanua Kiboye.

Wakati huo huo, Kibopye amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha njia na ujasiri wa kipekee katika kuhakikisha Watanzania kwa hiyari yao wanapata chanjo ya Corona.

"Niwaombe wananchi katika Mkoa wa Mara kujitokeza kushiriki zoezi la kupata Chanjo ya Uviko -19 pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari ili tuendelee kupambana dhidi ya Virus vya Corona.Niendelee kusisitiza, ndugu zangu wananchi na Watanzania kwa ujumla Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kuleta kitu huku akijua kina madhara, halafu akaanza kuchanja mwenyewe, hivyo niwaase tuzidi kujitokeza kuchanja chanzo hii ya Uviko-19,"aliongeza Kiboye.


Post a Comment

0 Comments