Tanzania Commercial Bank yaokoa wanafunzi 300 kukaa chini Mara, yatoa madawati 100

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB Plc) imekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa Shule ya Msingi Kenyamonta iliyopo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara ambapo wanafunzi 300 waliokuwa wakikaa chini sasa watakaa juu ya madawati na kusoma kwa ufanisi.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kenyamonta wakiwa wamekaa juu ya madawati yaliyotolewa msaada shuleni hapo na Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC)

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo shuleni hapo leo Agosti 13 2021,Meneja Mahusiano na Mawasiliano Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC), Chichi amesema kuwa,wamekuwa wakitenga bajeti ya kusaidia huduma mbalimbali katika jamii ikiwemo elimu na afya kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo kwa wananchi.

"Tunarudisha faida kwa njia mbalimbali ikiwemo kusaidia jamii kutatua kero za elimu na afya, lengo ni kuunga mkono Serikali yetu mkono. Tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka na ndio maana hata jana tulitoa madawati pia shule ya Msingi Maliwanda ' A' Wilaya ya Bunda lengo ni kuboresha mazingira yawe mazuri kwa watoto wanaposoma,"amesema Chichi.
Meneja Mahusiano na Mawasiliano Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC), Chichi Banda akizungumza wakati wa kukabidhi madawati 100 kwa shule ya Msingi Kenyamonta iliyopo Serengeti Mkoa wa Mara.Kulia kwake ni Meneja wa TCB tawi la Musoma Hagai Gilbert.

Aidha, Chichi amewataka walimu wa shule hiyo kusimamia utunzaji wa madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu. Huku pia akiwahimiza wazazi kushiriki kuchangia maendeleo badala ya kuiachia serikali pekee kutatua kila changamoto.

Meneja wa Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC) tawi la Musoma, Gilbert Hagai amesema kuwa,ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao wanahitaji mazingira bora ya kusomea na hivyo akasema ni imani yake kuwa madawati hayo yatainua ufaulu wa taaluma shuleni hapo.
Meneja Mahusiano na Mawasiliano Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC), Chichi Banda akiwa amekaa kwenye dawati la nyuma na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kenyamonta.Dawati la mbele ni Meneja wa TCB PLC tawi la Musoma, Hagai Gilbert mwenye tisheti ya bluu.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kenyamonta, Francisca Alphonce amesema kwamba, wazazi wengi katika kijiji hicho wamekuwa wakishindwa kuchangia maendeleo kutokana na uchumi wao kutegemea kilimo. Akasema TCB kutoa msaada huo umekuwa chachu ya ufanisi katika kuboresha elimu shuleni hapo.

Afisa Elimu wa Kata Kenyamonta, Machota Raphael Chacha amesema kutolewa kwa madawati hayo kunatatua tatizo kabisa la madawati shuleni hapo ambapo wanafunzi 300 waliokuwa wakikaa chini kwa sasa watakalia madawati hayo. Huku upungufu katika shule tano kati ya sita za msingi za serikali akisema zinakabiliwa na upungufu wa madawati 364 akaomba wadau kusaidia kutatua kero hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Kenyamonta, Henry Nyamate amesema Serikali inashukuru msaada huo kwani utakuwa na tija kubwa katika kuimarisha ufaulu na akaomba pia wadau wote kutorudi nyuma kusukuma mbele sekta ya elimu wilayani humo kupitia michango yao.

"Mkurugenzi wa Halmashauri ya Serengeti na Serikali kwa ujumla inashukuru msaada wenu (TCB) jukumu la kutatua tatizo hili limefanikiwa kupitia ninyi tunawashukuru sana. Niombe wadau wote waige mfano wenu na wajitokeze kushiriki kusaidia kero nyingi bado zipo, tusiiache Serikali ifanye kila jambo,"amesema Nyamate.

Dorcas Mwita ni mwanafunzi wa shule hiyo, ambapo amesema kuwa kutolewa kwa madawati hayo kunaondoa adha ya wanafunzi kuchafuka kwa kukaa sakafuni wakati wa masomo na hivyo wengine kushindwa kuhudhuria shule kutokana na mavazi yao kupata vumbi na kutakiwa kufua mara kwa mara.

"Wanafunzi wenzangu baadhi yao walikuwa hawaji shule kwa sababu wakija leo, kesho hawezi kuja mavazi yao yanachafuka kwa hiyo lazima wafue, kama mzazi hana hela ya sabuni hawezi kuja siku inayofuata kwa hiyo anakuwa mtoro kwa siku hata mbili,"amesema Dorcas.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kenyamonta Mujahiri Sidoro amesema kuwa, shule hiyo ina wanafunzi 736, ina upungufu wa meza 15 za walimu, viti 15 vya walimu, upungufu wa kabati 10 za kutunzia vitabu pamoja na upungufu wa mifuko 50 ya saruji na mabati 100 ili kukamilisha ujenzi wa Shule shikizi ya Bitare ambayo ina lengo la kuwaondolea adha wanafunzi kutoka Bitare kwenda kusoma Kenyamonta umbali wa kilomita tisa akaomba wadau na serikali kusaidia.
Meneja Mahusiano na Mawasiliano Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC), Chichi Banda akiwa na viongozi mbalimbali wakikata utepe wakati wa kukabidhi madawati 100 kwa shule ya Kenyamonta iliyopo Serengeti Mkoa wa Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news