TASAF kuifikia mitaa, vijiji 6,000 nchini, Mwanamke asimulia alivyorejeshewa tabasamu

Na Fresha Kinasa,Diramakini Blog

MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) Awamu ya Tatu kipindi cha pili unatarajia kuzifikia mitaa na vijiji vipatavyo 6,000 nchi nzima huku kaya masikini milioni 1,450,000 zikilengwa kutambuliwa na kuandikishwa ili ziingie kwenye mpango huo ambao utagharimu shilingi trilioni 2.03.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 10, 2021 na Swalehe Mwidadi ambaye ni mwezeshaji Kutoka TASAF makao makuu wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma mkoani Mara.

Ambapo zoezi la kuwaelimisha wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma waweze kutambua na kuandikisha kaya masikini ambazo zitanufaika na mpango huo linafanyika chini ya timu ya wataalamu kutoka TASAF makao makuu huku madiwani, watendaji wa kata na wataalamu wa halmashauri hiyo wakishiriki katika mafunzo hayo.

Mwidadi amesema kuwa, zoezi hilo litafanyika kwa umakini mkubwa na kwamba mpango huo utazigusa kaya masikini sana, huku akibainisha kuwa TASAF awamu ya tatu kipindi cha pili utagusa kaya zote zenye vigezo na vijiji vyote na mitaa upande wa Tanzania Bara pamoja na shehia zote upande wa Zanzibar.

"Mpango hautawagusa wazee, bali walengwa wenye sifa na vigezo. Mtu anaweza kuwa mzee ama mjane, lakini ana uwezo mtu huyo hataingia kwenye Mpango. Na pia Walengwa watalipwa kwa mfumo wa kielektroniki kwa hiyo Vitambulisho vya Taifa au namba za NIDA zitatumika kwa walengwa wote nchi nzima,"amesema Mwidadi.

Pia, Mwidadi aliwataka watakaoandikishwa na kuanza kunufaika na TASAF watumie fedha hizo kwa ufanisi kusudi ziwaletee mabadiliko chanya pindi wanapofuzu mpango huo. Badala ya kuzitumia kinyume na matakwa yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Mtaalamu Ufuatiliaji na Tathimini Kutoka TASAF Makao Makuu, Fariji Mishael alisema kuwa watakaonufaika na mpango huo ni wale watakaohudhuria vikao na mikutano itakayoitishwa na wataalamu kwenye kata, mitaa na vijiji ili kuwabaini na kuwatambua walengwa wakuu wa mopango huo.

Aliongeza kuwa, kwa wale wenye uwezo wa kufanya kazi watawezeshwa kupata ajira za muda itakayotekelezwa kwa kutumia nguvu kazi za walengwa hao na miradi iliyopo kwenye maeneo yao ambapo walengwa watafanya kazi siku kumi kwa miezi sita na kwa mwaka siku 60 huku wakifanya kazi kwa saa nne tu kwa siku ndipo ujira utalipwa kwa kazi kulingana na idadi ya siku alizoshiriki.

Pia alisema utoaji wa malalamiko umeboreshwa kwani kimetengenezwa kitabu maalumu cha kuandika malalamiko yao. Na vitabu hivyo vitakaa kwenye ofisi za watendaji wa kata na vijiji, lakini pia yatakuwa yakitolewa kwa njia ya mtandao ili kubaini idadi ya malalamiko yaliyotolewa eneo husika kwa njia ya simu namba 00800100057.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Justine Manko akizungumza kwa niaba ya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara alisema awamu iliyopita malalamiko yalikuwa mengi kutokana na uhaba wa elimu ya kutosha kuhusiana na walengwa halali wa mfuko huo. Akawahimiza waliopata elimu hiyo kuweza kuwaelimish wananchi kuhusiana na mpango huu ambao utakwisha mwaka 2023.

"Viongozi lazima mtambue walengwa halali watakaostahili kuingia kwenye mpango na ushirikiano uwepo kusudi walengwa wapate haki stahiki bila udanganyifu,"alisema Manko.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma aliwaasa madiwani na watendaji wote waliohudhiria mafunzo hayo, kutenda haki wakati wa zoezi la kuwatambua walengwa na kuwaandikisha katika maeneo yao ili kupunguza malalamiko ambayo yanaweza kudhoofisha ufanisi wa zoezi hilo.

Hilda Jackson (48) ni mkazi wa Kata ya Nyamatare Manispaa ya Musoma akizungumza na DIRAMAKINI BLOG amesema, anaipongeza TASAF kwani ameweza kusomesha watoto wake watatu wakahitimu kidato cha nne huku mmoja wao yupo Chuo Kikuu akisomea fani ya Uhasibu.

Amesema,kabla ya kuingia kwenye mpango hakuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto wake kwani mmewe alifariki dunia mwaka 2010 ambapo kwa sasa anamudu mahitaji ya familia yake kutokana na kujikita katika ujasiriamali wakati akiwa kwenye mpango.

Akashauri watakaoingia kwenye Mpango Awamu ya Tatu kipindi cha pili wawe wabunifu kwani siku moja watatoka na hivyo wawe na kitu cha kujivunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news