TRA Mkoa wa Mara yatoa wito kwa wafanyabiashara

Na Fresha Kinasa, Musoma

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imesisitiza wafanyabiashara mkoani humo kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu pamoja na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kuondokana na adhabu ambazo zinaweza kuwapata na kuathiri mitaji yao kwa kukwepa kodi.
Afisa Elimu Mwandamizi na Huduma kwa Mlipakodi Mkoa wa Mara, Zake Wilbard. (Picha na Diramakini Blog).

Hayo yamesemwa Agosti 23, 2021 Mjini Musoma na Afisa Elimu Mwandamizi na Huduma kwa Mlipa Kodi wa (TRA) Mkoa wa Mara, Zake Wilbard wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Manispaa ya Musoma wakati wa kikao cha pamoja kilichoandaliwa na mamlaka hiyo kwa lengo la kuwapa mabadiliko ya Sheria ya Kodi kwa mwaka 2021/ 2022 ambapo pamoja na mambo mengine, walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kujibiwa.

Zake amesema kuwa, Serikali inahitaji kufanya shughuli mbalinbali za maendeleo hivyo inahitaji fedha ambapo wafanyabiashara wakilipa kodi kwa uaminifu shughuli hizo zitatekelezeka kwa ufanisi. Huku akiwaonya kutojihusisha na ukwepaji wa kodi kwani wakibainika watatozwa faini na kupewa adhabu jambo ambalo hudhoofisha mitaji yao na kuwarudisha nyuma.

"Wafanyabiashara walipe kodi kwa hiari kusudi Serikali ipate fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo. Ukwepaji haufai niwaombe wafanyabiashara wazingatie ulipaji wa kodi kwa wakati pamoja na kutoa risiti baada ya kutoa huduma kwa wateja.Sambamba na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni kwa usahihi," amesema Zake.

Akijibu maswali ya wafanyabiashara mbalimbali waliotaka kujua kuhusu kodi ya ulipaji majengo kwa njia ya Luku alisema kuwa, kodi hiyo inatozwa kwa mwaka na inahusisha majengo yote ya kudumu. Huku akisisitiza kuwa kodi hiyo inapaswa kulipwa na mwenyenyumba na endapo mpangaji atalipia akinunua umeme anapaswa kuwasiliana na mwenye nyumba ili amrejeshe fedha yake na kuainisha mita moja itakayokuwa inakatwa kodi hiyo kila mwezi.

Zake aliongeza kuwa, kwa nyumba zilizounganishiwa umeme mteja atalipa atakaponunua umeme TANESCO na kwa wateja ambao hawana umeme wanapaswa kufika ofisi za TRA kupata ankara ya malipo na kulipia benki au kwa njia ya simu.

Na pia akasema kwa nyumba ya kawaida malipo kwa mwaka yatakuwa shilingi 12,000, ambapo kwa mwezi itakuwa na shilingi 1000 na kwa ghorofa kwa mwaka itakuwa shilingi 60,000 kwa kila sakafu kwa mwaka ambapo italipwa shilingi 5,000 kwa kila sakafu kila mwezi.

Akizungumzia kuhusiana na utaratibu wa kupata msamaha iwapo unaendelea Zake alisema kwa mtu yeyote anayemiliki jengo na aliyekidhi vigezo na masharti ya msamaha wa kodi ya majengo kwa mujibu wa sheria ataendelea kupata msamaha huo. Huku mnufaika ambaye atalipia umeme kimakosa atatakiwa kufika TRA akiwa na nyaraka husika na namba ya mita atasaidiwa na kiasi alicholipa kitawekwa kwenye umeme.

Pia, amesema kodi hiyo italipwa mara ya kwanza kila mwezi mteja anaponunua umeme na kwamba, baada ya hapo mteja hatatozwa iwapo atanunua umeme ndani ya mwezi endapo alinunua umeme sawa au unaozidi kiwango cha kodi hiyo ya majengo.

Mathias Pius ni mfanyabiashara katika Manispaa ya Musoma aliiomba Serikali kuliangalia upya suala hilo ili kuondoa migogoro baina ya wapanga na wamiliki wenyenyumba wasiowaelewa.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara, Boniphace Ndengo akiongea na wafanyabiashara wa Manispaa ya Musoma katika kikao kilichoitishwa na TRA mkoani humo kuhusu sheria Mpya za Kodi kwa mwaka 2021/2022. (Picha na Diramakini Blog).

Post a Comment

0 Comments