Utumishi yamkabidhi Mkandarasi kazi ya ujenzi jengo kubwa

Na Veronica Mwafisi,Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael amekabidhi kiwanja kwa Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi Watumishi Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma litakaloongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa umma.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akikabidhi kiwanja kwa mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi Watumishi Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akikabidhi eneo hilo kwa Mkandarasi, Dkt. Michael amesema, ofisi yake imepewa eneo jingine kubwa zaidi ya lile la awali ili kuwezesha ujenzi wa jengo la ghorofa sita lenye uwezo wa kutumiwa na watumishi 380 kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo, Dkt. Michael amesema kuwa, anatarajia Mkandarasi ataanza ujenzi mapema iwezekanavyo kwa kasi na kiwango kinachotakiwa ili kukamilisha ujenzi kwa wakati kama mkataba unavyojiainisha.

“Tunatambua kwenye taratibu za uhandisi huwa kuna hatua zinazozingatiwa, hivyo naamini taratibu hizo zitazingatiwa ipasavyo, msiharakishe kumaliza ujenzi halafu jengo likawa na mapungufu”, Dkt. Michael amesisitiza.
Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu Majengo wa WHC akimuahidi Dkt. Francis Michael usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.
Baadhi ya Wataalam wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Watumishi Housing Company (WHC) wakiwa katikati ya eneo la kiwanja walichokabidhiwa kujenga Jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Cosmas Ngangaji akihimiza ufanisi wa utendaji kazi kwa Mkandarasi (TBA) na mshauri Mwelekezi (WHC) waliopewa dhamana ya ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu Majengo wa WHC amemshukuru Dkt. Francis Michael kwa kuwakabidhi eneo kwa ajili ya kuanza usimamizi rasmi wa ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali, na kuongeza kuwa watahakikisha jengo linajengwa kwa kiwango na linakamilika kwa wakati.

Jengo hilo kubwa la ghorofa sita la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora linaloanza kujengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 7912 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 hadi 24.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news