Watalii 137 kutoka Israel wawasili Tanzania ikiwa ni kundi la pili

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mamia ya Watalii kutoka nchini Israel wameendelea kuwasili nchini Tanzania kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini.

Hayo yamethibithishwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete ambapo amesema, kundi la pili la watalii 137 kutoka Israel wamewasili nchini.

Shelutete amesema kuwa, watalii hao watakuwepo nchini kwa siku saba ambapo kundi la awali la watalii 150 kutoka Israel wameliza salama utalii wao nchini.

"Wageni wetu hao wamefurahia sana mapokezi yaliyoandaliwa kwa ajili yao, makundi mengine yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo,"amebainisha Shelutete.

Aidha, Watalii wengi wamenukuliwa wakisema kuwa wanakuja Tanzania kwa kuwa ni Taifa ambalo limebarikiwa vya kutosha kwa vivutio mbalimbali vya utalii na amani.

"Na wengi wameahidi kurudi tena huku wakisifu juhudi za Serikali kwa kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona (UVIKO-19) pamoja na tahadhari mbalimbali,"ameongeza.

Hivi karibuni, Shelutete alibainisha kuwa,ujio wa watalii hao ni matunda ya juhudi kubwa za utangazaji utalii zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Sambamba na jitihada za makusudi zinazochukuliwa na serikali hiyo katika kukabiliana na Corona kupitia miongozo inayoendelea kutolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ikiwemo kuhamasisha na kutoa chanjo ya ugonjwa huo.

Pia alibainisha kuwa,kuwepo kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Israel nako kumechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii kutoka nchini humo.

Ripoti zinaonyesha kuwa, Tanzania kwa mwaka jana ilipokea watalii zaidi ya 1,000 kutoka nchini Israel waliokuja kutembelea vivutio mbalimbali huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi.



Sehemu ya watalii 137 waliowasili nchini Tanzania kutoka Israel kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini. (Picha na TANAPA/Diramakini Blog).


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news