Waziri afanya ziara ya kushtukiza alfajiri ya leo Dodoma, azungumzia UVIKO-19

Na Abubakari Akida, MOHA

Serikali imewataka abiria wanaosafiri mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya UVIKO -19 huku wakiaswa kupaza sauti zao pindi wanapoona uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo alipofanya ziara, alfajiri ya kuamkia leo, lengo ikiwa kutoa tahadhari kwa wadau wa vyombo vya usafiri juu ya tahadhari ya ajali wawapo barabarani sambamba na kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kwa abiria hao.

“Sasa kuna janga la UVIKO-19 nawaomba muwe makini mkiwa safarini,vaeni barakoa na tumieni vitakasa mikono lakini pia nawaomba mpaze sauti zenu pindi muonapo uvunjifu wa sheria za usalama barabarani,nchi hii inawategemea sana katika kuleta maendeleo na serikali haipendi kuona watu wake wakipoteza viungo na Maisha,askari wetu wako kila sehemu huko barabarani toeni taarifa” alisema Naibu Waziri Chil

Akizungumzia madereva wanaoenda mwendokasi bila kufuata sheria za usalama barabarani Naibu Waziri Chilo alisema tayari serikali ishaanza utaratibu wa kuchukua leseni ya udereva kwa dereva yoyote atakaethibitika kusababisha ajali kwa uzembe wake.

“Hivi karibu mmeona jinsi dereva wa basi la Sauli linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tunduma alivyoyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari sasa ile ni hatari, ametokea Mbeya mbali kweli anakuja kupata ajali Kibaha alikuwa na haraka gani? tayari serikali kupitia mamlaka husika ikiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbrod Mutafungwa tushachukua leseni yake na tumemfungia kwa muda wa miezi sita na sasa atarudi darasani akajifunze upya udereva, kwenye kulinda maisha ya wananchi hatutaki mchezo” alisema Naibu Waziri Chilo.

Akizungumza kwa niaba ya madereva wengine, Dereva wa Basi la Al Saedy, Alex Emmanuel aliomba elimu itolewe kwa madereva wa malori kwani ndio wamekua chanzo cha ajali nyingi za barabarani hali inayopelekea kutokukoma kwa matukio ya ajali huku Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Boniface Mbao akiweka wazi kuwepo kwa utaratibu wa wa utolewaji wa elimu na ukaguzi wa mabasi kabla ya kuanza safari na basi linalokutwa na hitilafu basi huzuiwa lisiondoke.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news