Waziri Aweso avunja kamati ya maji, viongozi wakamatwa

Na Robert Kalokola,Geita

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amevunja Kamati ya Maji ya Jumuiya ya Watumia Maji ya Kijiji Mharamba,Kata ya Nkome wilayani Geita baada ya kubaini dalili za ubadhirifu katika makusanyo ya maji katika mradi wa Mharamba.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wanawake waliokuja kuchota maji katika kituo cha maji Katika Kijiji Cha Nyambaya Kata ya Katoma Wilaya ya Geita,kushoto ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Geita,Jabiri Kayila(Picha na Robert Kalokola).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bastaye Malima alimueleza Waziri wa Maji kuwa kamati hiyo ina laki 5 benki,lakini baada ya mahojiano na Waziri ikaonekana kamati ilipaswa kuwa imekusanya zaidi ya Milioni 20.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Bastaye Malima alisema kila wiki wanauza matenki ya maji matatu ambayo kila tanki wanapata 140,000.

Baada ya ufafanuzi huo wa Mwenyekiti wa kamati kuuza tanki 3 ambazo ukizidisha kwa kila mwezi na kwa mwaka ilionekana kamati hiyo ulistahili kuwa imekusanya zaidi ya Milioni 20 kwa mwaka mmoja.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso alilazimika kuvunja kamati hiyo na kuelekeza Ruwasa kwa kushirikiana na Mbunge kuunda upya Kamati hiyo yenye watu wenye uadilifu ili kuwezesha kuendesha mradi huo kwa tija zaidi.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo ameagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita na Takukuru kuwakamata Mwenyekiti,katibu na Mwekahazina wa kamati hiyo ili kufanya uchunguzi wa mapato na matumizi ya mradi huo.

Waliokamatwa na Jeshi la Polisi pamoja Takukuru kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo kwa ajili ya uchunguzi ni Mwenyekiti wa kamati Bastaye Malima, Katibu wa kamati Vedastus Magayane na Mwekahazina Mekitrida Silivanus.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Geita, Sande Batakanwa amesema kuwa Mradi huo ulianzishwa kujengea Mwaka 2013 na kuanza kutumika mwaka 2015.

Ameeleza kuwa mradi huo ulikuwa na bajeti ya Bilioni 1.2 lakini ulikamilika kwa gharama ya Bilioni 1.1 ambao una vituo vya kuchotea maji 20 lakini hadi Sasa vituo 17 ndivyo vinatoa maji na 3 vitakamilika muda si mrefu.

Aidha ameongeza kuwa mradi huo unatoa huduma kwa vijiji vya Mharamba kata ya Nkome na Nyambaya katika kata jirani ya Katoma ukiwa umelenga kuhudumia wananchi 4,000.

Waziri wa Maji Juma Aweso yuko katika ziara ya kutembelea miradi ya maji katika Wilaya ya ambapo ametembelea mradi huo na kuagiza Ruwasa Geita kuhakikisha inaandaa utaratibu wa kuunganishia wananchi maji kwenye nyumba zao kwa gharama nafuu kwenye kata hizo mbili.

Post a Comment

0 Comments