ALAT Tanga yataka Diwani alipwe posho Milioni 1/- kwa mwezi

Na Yusuph Mussa, Tanga

JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Tanga kwa kauli moja, imepitisha hoja ya kutaka Diwani kulipwa posho ya sh. milioni moja kwa mwezi, kwani itamsaidia yeye kujikimu kimaisha pamoja na kuwasaidia wananchi wake wenye shida mbalimbali ukichukulia yeye ndiye yupo karibu na wananchi kuliko Mbunge na Rais.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga Sadick Kallaghe akizungumza kwenye kikao cha ALAT cha mkoa huo. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga Abdulrahman Shiloow (kushoto) na Katibu wa ALAT Mkoa wa Tanga Halfan Magani (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).

Lakini pia wamejenga hoja kuwe na Mfuko wa Kata kama ilivyo Mfuko wa Jimbo ili kuweza kuchochea maendeleo kwa wananchi sababu madiwani ni wengi, na ndiyo wanakwenda hadi kwenye vitongoji kuhimiza shughuli za maendeleo, ambapo hoja zote mbili wataziwasilisha kwenye Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa utakaofanyika Dodoma Septemba 27-29, mwaka huu.

Hayo yalisemwa Septemba 20, 2021 kwenye Mkutano wa ALAT Mkoa wa Tanga, huku wajumbe wakichangia kwa kusema Madiwani nao wanatakiwa kuangaliwa maslahi yao kwa mapana ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na heshima tofauti na sasa, kwani wameonekana wanapata heshima kubwa kwa kuitwa waheshimiwa, lakini kwenye maslahi wanazidiwa na watendaji wa vijiji.

Diwani wa Kata ya Tanganyika, Wilaya ya Muheza Shafii Chewaja alisema wamepokea mapendekezo ya Kamati ya Utendaji ya ALAT Mkoa, na kusema ni maono makubwa yenye mashiko kwa mustakabali wa nchi na wananchi, kwani diwani amekuwa anafanya kazi kwenye mazingira magumu. Hata pesa anazotumia diwani, asilimia 80 ni pesa yake ya mfukoni, hivyo umefika wakati diwani apewe sh. milioni moja kwa mwezi badala ya 350,000.
Wajumbe wa ALAT Mkoa wa Tanga wakiwa kwenye kikao. (Picha na Yusuph Mussa).

Diwani wa Kata ya Nguvumali ambaye pia ni Mstahiki Meya Mstaafu wa Jiji la Tanga Mustapha Seleboss, alisema wanaomba posho ya mwezi ya diwani ifanane na hadhi yao, kwani huenda baadhi ya migogoro ama kutoheshimiana kati ya madiwani na watendaji, inatokana na posho ndogo ya madiwani.

"Posho ya diwani kwa mwezi ni sh. 350,000 huyo Mkurugenzi atakuheshimu vipi! Mtendaji wa Kata ama wa Kijiji mshahara wake ni sh. 800,000 wewe diwani atakuheshimu vipi! Naunga mkono hoja ya posho ya diwani kuwa sh. milioni moja kwa mwezi, kwani angalau itatufanya tuwe na hadhi ya kuitwa waheshimiwa. Lakini pia sisi tunafanya kazi ya Rais na Mbunge, sababu Rais hafiki hadi kwenye vitongoji" alisema Seleboss.

Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mwanaid Gogo alisema madiwani wanafanya kazi nyingi kwenye jamii ikiwemo kuwasaidia wagonjwa kufika kituo cha afya ama hospitali ya wilaya kwa kuwapa nauli. Lakini pia kama madiwani waliotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wana jukumu la kuwasaidia nauli viongozi wa chama ngazi ya kata na vijiji kwenda wilayani zaidi ya kilomita 60.

"Tunadharauliwa na watendaji wa vijiji kuwa huyu ni mtu wa maneno tu, lakin kwenye mshahara hawatuzidi. Sisi kila siku tunagongewa milango na wananchi wenye shida wakitaka kusaidiwa kwa shida mbalimbali ikiwemo zinazohitaji fedha. Bado viongozi wa chama wakienda wilayani karibu kilomita 60, unatakiwa umpe nauli wewe. hivyo sh. 350,000 ndogo... twende kwenye milioni moja" alisema Gogo.
Viongozi wa ALAT Mkoa wa Tanga wakiwa kwenye kikao. (Picha na Yusuph Mussa).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Amani Kasinya alisema anaomba Serikali Kuu na wabunge kuweza kuwatetea madiwani, kwani kwenye Uchaguzi Mkuu wao ni sehemu ya wagombea wanaopigiwa kura, hivyo baada ya kupita kwenye uongozi, waendelee pamoja badala ya kuwaacha njiani.

"Kwenye hiyena hiyena (Kampeni za Uchaguzi Mkuu) tupo mafiga matatu, lakin baada ya ushindi, figa moja linapigwa teke. Ndiyo najiuliza ni kwa nini niliemsaidia ashinde (Mbunge), posho yangu ya mwezi yeye ni posho yake ya kikao chake cha siku moja. Mwenyeviti wa Halmashauri kupewa gari kwenda kwenye msiba ni hisani ya Mkurugenzi, itategemea siku hiyo Mkurugenzi ameamkaje. Lakin sifa za Mwenyekiti huko mtaani utasikia, Mwenyekiti hii ni Halmashauri yako, wewe ndiyo mkibwa,"amesema Kasinya

Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahamn Shiloow alisema nia yao ni kuunganisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) na Serikali Kuu ili kuona zinafanya kazi kwa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja, kwani kama hawatafanya kazi kama timu moja, watashindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Shiloow ambaye ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwenye uchaguzi ujao, amewataka madiwani na watendaji kwenye MSM kufanya kazi kwa nidhamu, uwajibikaji na kuheshimiana ambako kutaleta ufanisi kwenye utendaji wa kila siku.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe aliunga mkono hoja ya kuanzishwa Mfuko wa Kata, kwani mfuko huo utaongeza nguvu kwenye miradi ya maendeleo ambapo fedha hizo zitaweza kupunguza kero ndogo ndogo za wananchi kama kumalizia ujenzi wa vyoo vya shule, kukamilisha ujenzi wa ofisi za vijiji, vitendea kazi (shajala) za ofisi na miradi ya wananchi.

"Jimbo la Korogwe Vijijini kwa mwaka linapokea sh. milioni 57 za Mfuko wa Jimbo. Kwa jimbo lenye Kata 29, vijiji 118, vitongoji 610 na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mombo, fedha hiyo sh. milioni 57 haitoshi. Diwan ambaye ana jimbo dogo angalau angepewa fedha sh. milioni tano hadi 10 ili awe na uwezo wa kununua mifuko 10 ya saruji kwa wananchi wake, pia ingesaidia kusaidia na Mfuko wa Jimbo kuleta maendeleo ya haraka.

"Ni kweli, posho ya madiwani kwa sasa haitoshi. Posho hiyo kwa sasa ni sawa na sh. 11,000 kwa siku. Tunataka iwe 30,000 kwa siku sawa na sh. milioni moja kwa mwezi. Posho hiyo itaongeza ari ya utendaji kwa madiwani na kuweza kuhudumia jamii yao kwa mapana zaidi," amesema Kallaghe.

Kallaghe ambaye pia anagombea Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ALAT Taifa, alisema mapato ya halmashauri ndiyo uti wa mgongo, hivyo Wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, washirikiane na madiwani na watendaji kuona mapato ya ndani ya halmashauri yanakusanywa. Na ili kufikia azma hiyo ni lazima kuwe na uadilifu katika kukusanya mapato hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news