Bodi ya Nishati Vijijini yamtaka Mkandarasi alipe madeni ya wananchi

Na Veronica Simba-REA, Shinyanga

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imemtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Ujazilizi mkoani Shinyanga, Kampuni ya Sagemcom kuwalipa wananchi wanaomdai kutokana na kazi mbalimbali walizofanya ikiwemo kuchimba mashimo ya kusimika nguzo za umeme katika Kijiji cha Bubiki, wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (kulia), akisalimiana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mwandu Fimbo wakati Bodi ilipowasili katika eneo hilo ikiwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 7 mwaka huu. Wa pili – kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga. (Picha na Veronica Simba-REA).
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Ujumbe wake wakiangalia Vibali vya kufanya kazi nchini vya Kampuni ya Ukandarasi Sagemcom kutoka Ufaransa inayotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani Shinyanga. (Picha na Veronica Simba-REA).

Agizo hilo lilitolewa Septemba 7 mwaka huu na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo wakati wa ziara ya Bodi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Maelekezo hayo ya Mwenyekiti yalitokana na madai ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Mwandu Fimbo kuwa Mkandarasi husika hajawalipa wananchi wa eneo hilo waliofanya kazi mbalimbali katika Mradi unaoendelea kutekelezwa mkoani humo.

Akifafanua, Fimbo alieleza kuwa pamoja na kuchimba mashimo ya kusimika nguzo za umeme, wananchi wanadai madeni mengine kufuatia huduma mbalimbali walizompatia Mkandarasi ikiwemo kodi ya nyumba aliyopanga.
Miundombinu ya umeme katika Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini. (Picha na Veronica Simba-REA).
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mwandu Fimbo (kushoto) akimwongoza Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo kukagua miundombinu ya umeme katika eneo hilo. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi. (Picha na Veronica Simba-REA).

Kufuatia hali hiyo, Wakili Kalolo alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga kusimamia suala hilo ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao mapema iwezekanavyo.

Akizungumzia suala hilo, Mhandisi Maganga alitoa muda wa wiki moja kwa Mkandarasi kuwa amelipa madeni yote ya wananchi hao vinginevyo Wakala utachukua jukumu la kumlazimisha kulipa kwa kukata malipo yake ya kazi ya usambazaji umeme na kuwapatia wananchi wanaomdai.

“Tumechukua namba ya Mwenyekiti wa Kitongoji na tutafuatilia. Endapo Mkandarasi atakaidi agizo hili, dhamana hiyo tutaichukua sisi wenyewe kwa kumkata malipo yake ili tuwalipe wananchi,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mwandu Fimbo (wa pili-kulia), akizungumza na Ugeni wake ambao ni Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) ukiongozwa na Mwenyekiti Wakili Julius Kalolo (kulia) aliyefuatana na Mjumbe Oswald Urassa (kofia nyeusi-katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga (kushoto). Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi. (Picha na Veronica Simba-REA).
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mwandu Fimbo (wa pili-kushoto), akizungumza na Ugeni wake ambao ni Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) uliokuwa katika ziara ya kazi, Septemba 7, 2021 kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini. (Picha na Veronica Simba-REA).

Kwa upande wake, Mkandarasi husika aliahidi kufanyia kazi maelekezo aliyopewa ambapo REA TANZANIA ilishuhudia akiwasiliana na Mwenyekiti wa Kitongoji kupata orodha ya majina ya wanaoidai Kampuni ili aanze utekelezaji.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi alifuatana na Mjumbe Oswald Urassa, Mkurugenzi Maganga pamoja na viongozi na wataalam mbalimbali kutoka REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news