Maagizo ya Naibu Waziri Dkt.Mabula kwa watumishi Sekta ya Ardhi

Na Hassan Mabuye, Dodoma

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka watumishi wa sekta ya ardhi wa mkoa wa Dodoma kuongeza kasi ya uandaaji na utoaji hatimiliki za ardhi kwa wananchi.
Dkt.Mabula ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki hii wakati alipokutana na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya ya Kondoa, Chemba, Bahi na Chamwino katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya sekta ya ardhi katika wilaya hizo za mkoa wa Dodoma.

Ameelekeza, kila ofisi ya halmashauri katika mkoa wa Dodoma kuandaa na kutoa angalau hatimiliki za ardhi 100 kila mwezi kwa kuwa kuna baadhi ya halmashauri ambazo amezitembelea na amekuta zinatoa zaidi ya hatimiliki za ardhi 300 katika kila mwezi.
“Huwezi kuwa na lengo la kuandaa hati 120 kwa mwaka, haiwezekani hata kama kungekuwa na mtumishi mmoja, haiwezekani. Nendeni mkapitie upya malengo yenu, labda mgeniambia haya ni malengo ya miezi mitatu sawa lakini sio malengo ya mwaka mzima,”alisema.

Naibu Waziri Mabula alitoa muda wa hadi kufikia tarehe 21 Oktoba 2021 halmashauri hizo zijipange kuanza kuoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za umiliki wa ardhi kwa hati na amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma kufuatilia kwa karibu.

Aidha, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Thadei Kabonge amewataka watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Dodoma kuepuka kuzalisha migogoro mipya hasa ile migogoro ambayo inazalishwa na uzembe wa watumishi wenyewe kwa kuwa inachangia katika kuchelewesha umilikishaji wa ardhi kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma, Swaumu Muganyizi amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuwa waadilifu na kuboresha utowaji huduma kwa wananchi na kuepuka rushwa hasa katika umilikishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news