Mashabiki Simba SC waridhika na viwango vya wachezaji wao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Baleke Jean dakika ya 84 ameitumia kuwapa TP Mazembe ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Simba SC.
Ni katika tamasha la Simba Day Septemba 19,2021 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Tamasha hilo ambalo lilijaza maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo kutoka maeneo ya Msimbazi, licha ya kufungwa wameonekana kuridhika na kiwango cha wachezaji wao.

Kwa nyakati tofauti wamemweleza MWANDISHI DIRAMAKINI kuwa, msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania na mechi zote za Kimataifa wanakwenda kufanya makubwa.

Pia wamewapongeza viongozi wa klabu hiyo, kwa kumchomoa mchua misuli wa Yanga FC, Farid raia wa Afrika Kusini.

Awali, Farid alionekana katika tamasha la Simba Day na kutambulishwa miongoni mwa viongozi wanaounda benchi la ufundi.

Wakati mechi inataka kuanza Farid pia aliongozana na benchi la ufundi na kwenda kukaa nao pamoja kwenye sehemu yao maalum.

Farid amedumu na Yanga SC kwa misimu miwili akitoa huduma ya kuchua misuli kwa wachezaji.

Awali upande wa Simba kulikuwa hakuna mchua misuli bali walikuwa na Adel Zrane ambaye yeye ni mtaalamu wa viungo.

Hata hivyo, Farid alipokuwa Yanga alikuwa na kitanda maalum ambacho alikuwa anatumia kuchua misuli wachezaji wa klabu hiyo.

Post a Comment

0 Comments