SERIKALI YAAHIDI KUKUZA UCHUMI WA WANANCHI

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, hivyo kila Mtanzania afanye kazi kwa bidii.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mti baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa mjengo ya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Karagwe, Septemba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Sasa tunakwenda kusimamia maboresho ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, Watanzania wote kila mmoja katika eneo migodini, viwandani, wavuzi, wakulima, wasomi na wafanyabiashara wafanye kazi kwa bidii ili kujiongzea tija;

Ameyasema hayo Septemba 19, 2021 wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo wilayani Karagwe, Kagera akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Rais Mheshimiwa Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika kila halmashauri. Vyuo hivyo vinatoa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha vijana hao kujiari au kuajiriwa.
Moja kati ya majengo yanayojengwa na serikali katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Karagwe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi na ukarabati wa majengo katika Chuo hicho Septemba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema mafunzo hayo ambayo yatakuwa yanatolewa katika taaluma za TEHAMA, ufundi umeme, makenika, ushonaji nguo, utawawezesha vijana wa Kitanzania kujiari au kuajiriwa. “Hatua hii itawakwamua kiuchumi na kuwaondoa katika utegemezi, huu ndio mkakati wa Rais Mheshimiwa Samia.”

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao unagharimu shilingi bilioni sita na kumuagiza mkandarasi anayenga ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania ahakikishe anaukamilisha kwa wakati ili malengo ya Serikali yaweze kutimia.

Mradi huo unahusisha ukarabati majengo matano na kujenga majengo mapya manane ambayo ni kubadilisha jengo la utawala kuwa madarasa, kukarabati karakana ya ushonaji, kubadilisha jengo la bohari na kuwa karakana ya ufundi wa zana za kilimo na ufundi bomba.

Pia, kubadilisha bohari ya vitu vya jumla (general store) kuwa karakana ya uchomeleaji na uungaji vyuma (welding and fabrication), kukarabati karakana ya ufundi wa magari (Motor Vehicle Mechanics Workshop).

Majengo yanayojengwa ni jengo la Utawala lenye Maktaba, Maabara ya “electronics” na Maabara ya Kompyuta, jengo la maliwato, jengo la Mafunzo ya ufundi mchanganyiko, jengo la bohari, jiko na bwalo la chakula, karakana ya ufundi umeme na hosteli ya wavulana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news