Mgongolwa: Rais Samia ameonyesha mfano, viongozi nanyi ondokeni ofisini

Na Mwandishi Wetu

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa amewashauri viongozi wote kuanzia ngazi za chini ndani ya chama na Serikali kuwa mstari wa mbele kushughulikia kero na changamoto zinazowakabili wananchi ili kuharakisha maendeleo.

Amesema,hatua hiyo itaongeza kasi ya kufikisha maendeleo maeneo yote nchini, ikiwa ni malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambayo imejipambanua wazi kutomuacha nyuma Mtanzania yoyote katika kuleta maendeleo nchini.

Pia amesema, kuna kila sababu kwa viongozi na watendaji wote ndani ya chama na serikali kushughulikia mambo mbalimbali ya wananchi badala ya kukaa ofisini.
Mgongolwa ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumza kuhusiana na namna ubunifu wa Rais Samia kwa ajili ya kuharakisha maendeleo nchini unavyopaswa kuigwa na viongozi wenye mamlaka.

"Ni hivi karibuni tu. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameondoka ofisini na kwenda kurekodi kipindi cha Royal Tour, kipindi mahususi kwa ajili ya kulitangaza Taifa letu kupitia vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini.

"Hatua ile ni ishara ya wazi kuwa, waliopewa dhamana hawapaswi kukaa ofisini muda wote. Badala yake watumie nafasi walizonazo kubuni mambo yenye maslahi mapana kwa Taifa na faida, sasa baada ya kile kipindi, tutarajie neema siku za karibuni katika Sekta ya Utalii, kwani wataanza kumiminika Tanzania, fursa za ajira na uchumi kustawi zitafunguka, hivyo ubunifu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni wa kupongeza sana,"amesema Mgongolwa.

Pia amewataka viongozi wa chama kuendelea kuhamasisha na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya shina hadi juu na kuhimiza mahusiano ndani ya chama pamoja na Serikali.

Mgongolwa amesema, Rais Samia anapaswa kuungwa mkono na kuendelea kuombewa na Watanzania wote kwani katika muda mfupi serikali anayoiongoza imetoa mwelekeo wenye matumaini makubwa ya kuimarisha ustawi wa wananchi.

Sambamba na uchumi wa nchi yetu, kuvutia uwekezaji zaidi, kuzalisha ajira kwa vijana na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu na raia wote.

Post a Comment

0 Comments