Jeshi la Polisi laonya wanaodai uwepo wa TELEZA Arusha

Na Abel Paul

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo leo Septemba 16, 2021 ametoa taarifa juu ya uvumi wa taarifa zinazoenea katika baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusiana na taarifa za mtu mmoja asiyefahamika jina halisi maarufu TELEZA kuingia katika nyumba zao nyakati tofauti tofauti kwa nia ya kutenda uhalifu.
Kamanda Masejo amesema kuwa, Jeshi la Polisi mkoani Arusha baada ya kupata taarifa hizo lilianza kufuatilia na kuwahoji watu wanaosadikika kuwa ni wahanga wa matukio hayo ambao walionekana katika baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa ni wahanga wa matukio hayo ya kuvamiwa na mtu wasiyemfahamu nyakati tofauti tofauti ndani ya nyumba zao huko maeneo ya Murieti Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Kamanda amesema kuwa, katika mahojiano imebainika kuwa watu hao hawafahamu kuhusiana na jambo hilo wala mtu huyo isipokuwa wamesikia mitaani kuhusiana na tuhuma hizo za mtuhumiwa huyo asiyefahamika sura wala jina halisi kuwa uingia kwenye nyumba nyakati za usiku.

ACP Masejo amesema, Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kupokea taarifa na kukamata wahalifu mbalimbali kuhusiana na makosa ya uvunjaji na ukatili dhidi ya wanawake katika maeneo ya Murieti na katika maeneo mengine katika Mkoa wa Arusha.

Ametoa rai kwa baadhi ya mitandao ya kijamii inayohoji na kutoa taarifa hadharani za watu wanaosadikika kuwa ni wahanga wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake,kuwa jambo hilo linafifisha usalama wa wahanga wanaohojiwa hadharani na mitandao hiyo na kutoa taarifa na ushahidi wa wazi na pia kwa kufanya hivyo kunadhohofisha upelelezi na ushahidi wa kesi katika mchakato wa kisheria vile vile kutawapa mwanya wahalifu kutumia kama fursa ya kufanya uhalifu na kutumia kivuli na tuhuma hizo kufanya uhalifu.

"Aidha, nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi ambalo litazifanyia kazi kwa wakati na kuzingatia usiri mkubwa,"amesema.

Post a Comment

0 Comments