NBC KUTOA MIKOPO KWA WACHIMBAJI WADOGO

Na Robert Kalokola,Geita

Wachimbaji wadogo wa madini nchini pamoja na wajasiriamali wadogo wataanza kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) baada ya kuanzisha utaratibu mpya wa kutoa mafunzo kwa wachimbaji hao ili watambue masharti nafuu ya kupata mikopo hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Tawi la Geita la Benki ya NBC, Hilda Bwimba katika maonesho ya uwekezaji na teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Ukosefu wa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wajasiriamali mkoani Geita kupata ugumu wa kupatiwa mikopo kutoka katika taasisi za fedha ili kukuza mitaji yao.

Hayo yamesemwa na Afisa Biashara kutoka Benki ya NBC Tanzania, Elvis Ndunguru mkoani Geita kwenye maonesho ya nne ya uwezekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita.
Meneja Biashara wa NBC,Elvis Ndunguru akizungumza katika banda la benki hiyo katika maonyesho ya Dhahabu mjini Geita (picha na Robert Kalokola)

Elvis Ndunguru amesema kuwa wachimbaji wadogo wadogo walikuwa hawapati mikopo kwa kukumbana na vikwazo mbalimbali katika Mabenki hivyo NBC imeandaa utaratibu maalum wa kuwapatia mikopo kwa masharti nafuu.

Meneja wa Biashara wa NBC, Elvis Ndunguru ameongeza kuwa, benki hiyo inatoa mikopo ya vitendea kazi ambavyo ni mitambo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo wadogo ambayo inatumika katika kuchimba madini.
Afisa wa Benki ya NBC Makao makuu akitoa huduma kwa mteja katika Banda la Benki hiyo kwenye maonesho ya uwekezaji na teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Amefafanua kuwa, kipindi cha nyuma wachimbaji wachimbaji wadogo walikuwa wanapewa vipengele vigumu vya kukidhi kupata mikopo hiyo, hatimaye benki ya NBC imeleta suluhisho kwa kuwapa mafunzo ya namna njema itayowafanya wapate mikopo bila masharti magumu.

Maonesho hayo ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini ni ya nne kufanyika mjini Geita. Lengo likiwa ni kukutanisha wadau mbalimbali katika mnyororo mzima wa uchimbaji madini.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Mkoa wa Geita wanaofanya kazi za uchimbaji wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, utaratibu huo wa NBC utawasaidia kuongeza mitaji yao na kuchimba kwa uhakika zaidi tofauti na kipindi cha nyuma ambacho ilikuwa ngumu kupata mikopo.
Maafisa wa Benki ya NBC wakimfungulia akaunti mteja katika banda la benki hiyo kwenye maonesho ya uwekezaji na teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Geita, Christopher Kadeo amesema kuwa maamuzi ya NBC kutambua mchango wa wachimbaji wadogo na kuanza kuwapa mafunzo na kutoa mikopo itakuwa mkombozi kwao kwa sababu walikuwa na kilio cha muda mrefu cha kukosa mitaji ya uhakika.

Ameongeza kuwa, taasisi nyingi za fedha zilikuwa hazitambui wachimbaji wadogo na walikuwa hawaaminiki katika taasisi hizo hivyo ilikuwa ngumu kupata mikopo kutoka taasisi hizo

Kwa Upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Geita (TCCIA) Kitengo cha Biashara, Betha Komba amesema, wameanzisha mpango wa kuwapa semina ya mafunzo ya kupata mikopo wajasiriamali mkoani humo wakishirikiana na taasisi za fedha ili kuwapa uelewa mkumbwa na kupunguza malalamiko ya vizuizi wanavyokutana navyo wakati wa kuomba mikopo hiyo.

Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa inayozalisha madini ya dhahabu kwa wingi hapa nchini ambapo inazalisha zaidi ya asilia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments